Tuesday, April 30, 2013

Bajeti ya maji yawa moto

Wakati serikali ikijikusanya huko na huko ili kuongeza bajeti ya  Wizara ya Maji kwa mwaka wa fedha wa 2013/2014 kutoka Sh. bilioni 398.4 zilizokuwa zimetengwa awali hadi Sh. bilioni 582.8, jana pia ilijikuta ikifurushwa kwenda kujipanga vema baada utoaji wa taarifa ya nyongeza hiyo kudaiwa kukiuka kanuni.

Hali hiyo ilitokea baada serikali kupitia kauli ya Waziri wa Fedha, William Mgimwa, kueleza jinsi nyongeza ya fedha hizo ilivyopatikana, lakini wabunge wakapinga utaratibu uliotumika.

Wabunge hao ni pamoja na Tundu Lissu (Singida Mashariki-Chadema) na John Mnyika (Ubungo-Chadema), ambaye alisema kwa jinsi mawaziri hao walivyotoa kauli za serikali, ni sawa na kuwauzia wabunge mbuzi kwenye gunia.

Walisema utaratibu wa mawaziri hao ulikiuka kanuni za Bunge namba 49 (3), 57 (2) na 100 (1) na kutaka kiti cha Spika kuchukua hatua, ikiwa ni pamoja na kuahirisha mjadala wa bajeti hiyo.

Kwa mujibu wa wabunge hao, kanuni hizo zinamtaka waziri kutoa nakala kwa wabunge kuhusu kauli ya serikali anayoitoa bungeni, jambo ambalo halikufanywa na mawaziri hao hata kwa Spika pia.

Akitoa Mwongozo wake, Spika Makinda, pamoja na mambo mengine, alisitisha mjadala wa bajeti hiyo jana asubuhi hadi katika kikao cha jana jioni ili kuipa serikali nafasi ya kwenda kujipanga vizuri.

Kabla ya kuahirisha kikao hicho, Makinda alisema kwa taarifa alizonazo ni kuwa fedha zilizoongezwa zimetoka katika mafungu ya posho katika wizara ambazo zimeshawasilisha bajeti yake.

Kutokana na udhaifu huo, Spika aliahirisha kikao cha Bunge asubuhi hadi jana jioni ili serikali ikatimize wajibu wake kwa mujibu wa kanuni.

Awali, serikali ilisema kuwa iliamua kuongeza fedha hizo ili kukabiliana na tatizo kubwa la upatikanaji wa maji nchini, hususan maeneo ya vijijini, lililolalamikiwa na wabunge.

Nyongeza hiyo inafuatia mapendekezo yaliyotolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, ambayo ilipendekeza kuongezwa Sh. bilioni 184.5 katika bajeti hiyo ili kukidhi mahitaji makubwa ya maji nchini.

Aidha, matumizi ya kawaida bajeti yake imeongezwa kutoka Sh. bilioni 18.9 hadi Sh. bilioni 29.6 huku fedha za matumizi mengine zikipungua kutoka Sh. bilioni 16 hadi Sh. bilioni tano.

Kadhalika, serikali imeonya kuwachukulia hatua kali maofisa wote wa wilaya watakaokwamisha utekelezaji wa miradi ya maji nchini, ikiwa ni pamoja na kuwafukuza kazi.

 Hata hivyo, wakati hayo yakijiri, baadhi ya wabunge kutoka upinzani wameonyesha wasiwasi wao kuhusu nyongeza hiyo kwa maelezo kwamba, kanuni za Bunge katika kutoa kauli hiyo ya serikali bungeni zilikiukwa.

Wakati Waziri Mgimwa akieleza nyongeza hiyo, Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, alitoa onyo hilo dhidi ya watumishi wa umma wanaosimamia sekta ya maji.

Waziri Mgimwa alisema serikali imelitazama tatizo lililokuwa likiikabili bajeti hiyo, kuangalia kwa umakini hoja za wabunge na kutazama umuhimu wa maji kwa wananchi.

Kutokana na hilo, alisema serikali imeona iungane na hoja za wabunge kwamba, tatizo la maji walipe kipaumbele zaidi.

Alisema jambo la pili, ni kwamba, katika kutoa kipaumbele zaidi kwa upande wa maji, serikali imelifanyia kazi suala hilo kiundani na kuangalia namna ya kupata fedha za ziada kwa kutazama mafungu mengine.

“Tumetazama kiundani na kuona mafungu mbalimbali ya posho, ambayo hayataathiri sana utendaji wa serikali yakipunguzwa, basi tuyapunguze mafungu hayo tuongeze fedha katika Mfuko wa Maji,” alisema Waziri Mgimwa.

 Jambo la tatu, alisema katika kuitekeleza kazi hiyo, wizara yake itawasilisha katika kipindi cha kuwasilisha Muswada wa Sheria ya Matumizi ili maeneo ambayo yatapunguzwa, yalete afueni kwa ajili ya bajeti ya maji yatakayoguswa.

Alisema jambo la nne, katika kutekeleza kazi hiyo, uchambuzi huo wa ndani atauwasilisha kwenye kamati husika ili wajumbe wake waone maeneo ambayo watayagusa ili kusaidia kuongeza mafungu ya maji.

Kwa mujibu wa Waziri Mgimwa, wamezingatia vifungu vilivyowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Maji na Mifugo, na kwamba, kiwango hicho ndicho walichokizingatia katika kuongeza bajeti ya Wizara ya Maji.

Baada ya kueleza hayo, Spika wa Bunge, Anne Makinda, alimtaka Waziri Mgimwa, kutaja kiwango cha fedha kilichoongezwa kwenye bajeti ya Wizara ya Maji.

Waziri Mgimwa alisema Mwenyekiti wa Kamati hiyo, baada ya kueleza kwa undani, alipendekeza ziongezwe Sh. bilioni 184.5 na kwamba, kiwango hicho ndicho kilichopendekezwa pia na wabunge wakati wakiijadili bajeti hiyo bungeni.

Waziri Maghembe alisema fedha za utekelezaji wa miradi ya maji zimeshapelekwa vijijini, utekelezaji wake utakamilika ifikapo mwaka 2019 na kwamba, asilimia 62 ya watu watapata maji nchini kote.

Alisema ifikapo Septemba, mwaka huu, watakagua wilaya na kwamba watachukua hatua, ikiwa ni pamoja na kuwafukuza kazi maofisa watakaoshindwa kutekeleza miradi ya maji.

Hata hivyo, alisema utekelezaji wa miradi ya maji si kazi ya ushabiki wa kisiasa, bali ni ya ujenzi wa miundombinu, hivyo haiwezekani kuandamana kwenda Wizara ya Maji kupewa glasi ya maji kwa siku moja.

Kuhusu teknolojia ya matumizi ya maji ya bahari kwa Dar es Salaam, alisema kumekuwa na maendeleo ya kuondoa chumvi kwenye maji hayo na kwamba, utafiti wake unaendelea.

Alisema ameunda kamati ya wataalamu itakayoongozwa na Makamu Mkuu wa chuo Kikuu cha Ardhi (Aru), Profesa Idrisa Mshoro, kufuatilia thamani ya miradi ya maji ili kudhibiti matumizi ya fedha nyingi za miradi hiyo na kwamba, serikali italipa visima vitakavyotoa maji na siyo ‘vikavu’.

No comments: