Thursday, April 25, 2013

Serikali yajibu madai ya Dk. Cyril Chami

Serikali imepinga hoja ya Mbunge wa Moshi Vijijini (CCM), Dk. Cyril Chami, kuhusu kasi ya maendeleo katika jimbo la Hai linalowakilishwa na Freeman Mbowe (Chadema).
 
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, amemtaka Dk. Chami kutambua kwamba Rais Jakaya Kikwete ni kiongozi wa Watanzania wote, hivyo utekelezaji wa ahadi zake hauingiliani na matakwa ya kisiasa.
 
Gama akizungumza na NIPASHE jana alisema Rais anapotekeleza ahadi alizoahidi haangalii jimbo fulani ni la mpizani au mbunge wa chama tawala bali jambo la msingi linaloangaliwa ni umuhimu wa kuhudumia wananchi wote.
 
“Siyo kweli kwamba kuna barabara zinazopendelewa, nasema habari ya kuingiza masuala ya siasa katika mambo haya siyo sahihi, barabara zote zilizoahidiwa na Rais zitajengwa kwa utaratibu ambao umepangwa na serikali,” alisema Gama.
 
Alisema wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro wasiwe na wasiwasi kwani barabara zikishatengenezwa hata kama zipo katika jimbo linaloongozwa na mbunge wa Chadema, lakini watapita wananchi wa vyama vyote.
 
Gama alisema mwaka  2010  Rais aliahidi barabara sita katika majimbo yaliyopo Mkoa wa Kilimanjaro ambazo baadhi zimeanza kutengenezwa na nyingine zipo katika mchakato.
 
Alisema  barabara ya Rau madukani-Mamboleo hadi Kishumundu inayolalamikiwa na mbunge kwamba imekuwa ikikarabatiwa kwa kuwekwa kifusi licha ya kwamba ilijengwa kwa lami ipo chini ya Halmashauri na mafungu ya kuitengeneza yamekuwa yakitolewa na halmashauri husika.
 
“Mbunge (Dk. Chami) ni mjumbe wa Bodi ya Barabara ya mkoa, hivyo masuala mengine yanatakiwa yazungumzwe kwenye vikao, na katika suala la utekelezaji wa ahadi hatuangalii miaka, mfano zipo barabara ambazo ziliahidiwa wa Rais mstaafu, Benjamini Mkapa, ambazo zinatekelezwa na Rais Kikwete,” alisema Gama.
 
Hatua ya serikali kutoa kauli hiyo imefuatia Dk. Chami kuandika barua kwenda Wizara ya Ujenzi akilalamikia ujenzi wa barabara ya lami katika Jimbo la Hai.
 
 Katika barua yake kwenda kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Gerson Lwenge ya Febrauari 4, mwaka huu, Chami anatoa mfano wa barabara ya Rau Madukani-Mamboleo-Kishumundu iliyopo Kata ya Uru Mashariki ilijengwa kwa kiwango cha lami mwanzoni mwa miaka ya 1970. 
 
Chami alisema barabara hiyo tangu wakati huo, ikiharibika haikarabatiwi kwa kurudishia lami bali hujazwa kifusi kitu ambacho anadai ni kinyume na taratibu za ukarabati wa barabara za kiwango cha lami. 
 
Alisema hali hiyo ni tofauti katika barabara ya Machine Tools kwenda Machame iliyopo Hai iliyojengwa miaka ya 1950 ambayo Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Kilimanjaro kila inapoharibika  hukarabati kwa kurudishia lami.
 
Chami katika barua yake alisema kinachoongeza utata ni barabara ya Machine Tools-Machame iko katika Jimbo la Hai ambalo linaongozwa na Chadema.
 
Alisema viongozi wa Chadema wanawakejeli wananchi wa Moshi Vijijini walioichagua CCM kuwa barabara yao (watu wa Hai) ya Machame inakarabatiwa kwa lami kwa sababu wao waliichagua Chadema na kwamba kinachoifanya barabara hii ya Moshi Vijijini ijazwe kifusi ni kwa sababu waliichagua CCM. 
 
Chami amebainisha kuwa kutokufanya hivyo ni kutoa kipaumbele zaidi kwa Chadema kuliko maeneo yanayoongozwa na CCM.

No comments: