Tuesday, April 30, 2013

Hati za wamiliki wa mashamba ya mkonge Muheza kufutwa

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imetangaza kuwa wakati wowote itakamilisha mchakato wa kufuta hati za mashamba ya mikonge yaliyotelekezwa katika Wilaya za Muheza na Kilindi mkoani Tanga.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Goodluck Ole-Medeye wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kilindi Dastan Kitandula (CCM).
Ole Medeye alisema kuwa uamuzi wa kufuta hati miliki hizo kwa sasa uko mikononi mwa Rais baada ya kukamilika kwa hatua zote.
Katika swali hilo Kitandula alitaka kujua ni lini Serikai itafuta hati miliki kwa mashamba ya mkonge ambayo kwa muda mrefu yametelekezwa ili kuwagawia wananchi wenye uhitaji.
Awali, Herbert Mtangi (Muheza-CCM) alitaka kujua ni viwango gani stahiki ambavyo wawekezaji wa zao la katani wanatakiwa kulipa kama ushuru kwa halmashauri husika.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Hawa Ghasia, alisema kuwa halmashauri zote nchini zimepewa mamlaka ya kutoza ushuru wa mazao chini ya kifungu 7 (1) (g) cha sheria ya fedha za serikali za Mitaa.
“Ushuru huu hulipwa na mununuzi na unatozwa mahali ambapo zao linazalishwa na kwa bei ya mkulima yaani bei ya zao kabla ya kuongezwa thamani,” alisema Ghasia.
Alisema wafanyabiashara wote wa zao la mkonge,wanatakiwa kulipa ushuru wa mazao ambao ni kuanzia asilimia 3 hadi 5 kwa mujibu wa sheria.
Wakati huohuo, Naibu Waziri wa Maji, Dk Binilith Mahenge amemtetea bosi wake, Profesa Jumanne Maghembe kuhusu tuhuma zilizoelekezwa kwake za kupeleka mradi mkubwa wa maji jimboni kwake, huku wilaya zingine zikiachwa ‘yatima’.
Akijibu hoja mbalimbali za wabunge jana, Dk Mahenge alisema mradi wa Mwanga-
Same-Korogwe ni mwendelezo wa miradi mikubwa ya maji kama ule wa Chalinze.
“Yote yaliyoelezwa tutayazingatia. Ni kweli kutokana na unyeti wa suala la maji, lazima hisia zitapelekea mawazo mengi juu ya kasungura kadogo kuonekana mtu mmoja amejimegea wengine hakuna,” alisema Dk Mahenge.

No comments: