Friday, April 26, 2013

Kibali cha kunikamata kitatoka kwa Spika: Lema

Jeshi  la Polisi linamsaka Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema kwa tuhuma za kuhusika katika vurugu zilizotokea juzi katika chuo cha Uhasibu Mkoani Arusha (IAA) na kusababisha chuo hicho kufungwa kwa muda usiojulikana.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoani Arusha, Ibrahim Kilongo, aliwaaambia waandishi habari kuwa jeshi hilo limetoa ilani kwa mbunge huyo kujisalimisha polisi haraka.
Wakati polisi wakisema hayo, Lema ameeleza kushangazwa na hatua ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha kutoa amri ya kumkamata.
Alisema kibali cha kukamatwa kwake ni lazima kitoke kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda.
Lema aliyasema hayo wakati akizungumza na waandishi jijini hapa na kuwa  atakamatwa ikiwa Spika Makinda atatoa kibali cha kukamatwa kwani yeye ni mbunge halali wa Arusha Mjini.
Pia aliwapa pole wanafunzi kwa msiba wa mwanafunzi mwenzao kisha kuwapa pole wanafunzi wengine waliokumbwa na kadhia ya kupigwa mabomu juzi eneo la chuo wakati wakidai haki zao za msingi ikiwamo kuhoji matukio ya vifo vya wanafunzi wenzao vinavyotokea mara kwa mara chuoni hapo.
Hata hivyo, kamanda Kilongo alisema: “Tunamtaka popote alipo afike mwenyewe  polisi na bado tunaendelea kumtafuta popote alipo, ni muhimu afike tufanye naye mahojiano kuhusu yaliyotokea katika chuo cha uhasibu."
Lema anatuhumiwa kuhusika katika vurugu zilizopekea kudhalilishwa na kuzomewa kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo.
Mara baada ya kutulizwa kwa vurugu hizo, Mulongo aliliagiza jeshi la polisi kumkamata Mbunge huyo kwa kile kilicholezwa kuwa ni kumhusisha na vurugu zilizotokea chuoni hapo juzi.
Katika tukio hilo lililosababisha mabomu ya machozi kurindima kwa kwa muda chuoni hapo, Mulongo alijikuta akizomewa baada ya kushindwa kuhutubia mamia ya wanafunzi.
Awali, Naibu Mkuu wa Chuo cha Uhasibu jijini Arusha, Faraji Kasidi, alisema chuo hicho kimebeba jukumu la kuusafirisha mwili wa mwanafunzi Henry Kago (22) na kuupeleka nyumbani kwao Iringa kwa ajili ya mazishi.

No comments: