Tuesday, April 30, 2013

Jaji Manento: Polisi wanabambikia kesi raia

Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji mstaafu Amiri Manento, amelituhumu Jeshi la Polisi nchini kuwa linawabambikiza kesi wananchi na kutumia nguvu nyingi kupita kiasi zinazosababisha vifo vya raia wasiokuwa na kosa.

Alisema jeshi hilo limeshindwa kufanya kazi kwa kuzingatia sheria na taratibu katika utendaji wa kazi wa kila siku na kwamba hatua hiyo inayochangia kuwapo kwa matukio ya mauaji ya raia katika maeneo mbalimbali nchini.

Aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam kwenye Jukwaa la Asasi za Kiraia zinazopinga adhabu ya kifo na kusisitiza kuwa polisi wanakiuka maadili katika utendaji wao wa kazi. Alisema  polisi wanaokiuka maadili ya kazi, lakini hawajawahi kuchukuliwa hatua zinazostahili na kwamba hali hiyo imekuwapo kwa kipindi kirefu.

Jaji Manento alilitaka jeshi hilo kufanya kazi kwa kufuata sheria za nchi na kwamba yeye na tume yake kazi yao ni kuhubiri amani na kwamba hawana mamlaka kisheria ya kukamata mtu yeyote.

Kuhusu Tanzania kufuta adhabu ya kifo, Jaji Manento alisema jambo hilo linahitaji muda na kwamba haiwezekani likafanyika kwa mara moja na kumalizika.

“Huwezi kuamka asubuhi na kusema umefuta adhabu ya kifo, badala yake uwe ni mchakato wa muda mrefu ambao mwisho wake utasaidia kuifuta na kuondokana nayo,” alisema.

Akizungumzia mauaji yanayofanywa na wananchi dhidi ya wenzao, Jaji Manento alisema tatizo hilo linatokana na watu kutokuwa na kazi maalum za kufanya na kwamba vijijini zinapofanyika shughuli za kilimo takwimu za mauji zipo chini ikilinganishwa na mijini.

Aliitaka jamii kujisikia vibaya mtu mmoja anapopoteza maisha kwa namna yoyote ile na kwamba ikifikia hapo inaweza kupunguza mauaji yanayofanywa na raia wenye hasira.

Kuhusu jamii kubadilika na kutii sheria, Jaji Manento alisema tume yake kwa kipindi kirefu imekuwa ikizunguka nchi nzima kutoa elimu ya namna hiyo ingawa bado vitendo viovu vinaendelea kufanyika maeneo mbalimbali nchini.

Mwanaharakati wa haki za binadamu kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Harold Sungusia, alisema adhabu ya kifo imeendelea kutolewa nchini licha ya kuwa tangu mwaka 1994, marais hawajawahi kutia saini ili waliohukumiwa wanyongwe.

Alisema hukumu ya kifo ni miongoni mwa sheria mbaya zinazotakiwa kufutwa kwa kuwa haitoi fundisho kwa mhusika badala yake inaongeza maumivu. Aliongeza kuwa umefika wakati serikali kuwa na adhabu mbadala badala ya kifo kwa kuwa tangu imeanza kutolewa tatizo halijaweza kumalizika katika jamii na kwamba matukio ya mauaji yameendelea.

Mmoja wa mtu aliyehukumiwa adhabu ya kifo na Mahakama Kuu na kuachiwa huru na Mahakama ya Rufaa, Michael Lembeli, alisema alikamatwa na polisi akiwa kidato cha nne mwaka 1994 na kubambikwa kesi ya mauaji. Alisema siku aliyokamatwa polisi walifika nyumbani kwao wakimsaka mpangaji wao waliyedai kamba aliiba mito ya makochi na baada ya kumkosa wakamkamata yeye, lakini cha kushangaza alipofika kituoni aliambiwa ameua ofisa wa Jeshi.

Alisema licha ya kubambikiwa kesi hiyo, lakini pia alipigwa na kulazimishwa kukubali kuandika maelezo polisi kwamba ameua ili aachiwe huru. Alisema baada ya kuyaandika, yalitumika mahakamani kama ushahidi na hivyo kumfanya atiwe hatiani na kuhumiwa kifo na Mahakama Kuu Kanda ya Tabora.

No comments: