Friday, April 26, 2013

Machinjio ya Ukonga yafungwa kwa uchafu

Mamilioni ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam huenda wakakabiliwa na uhaba wa kitoweo kufuatia hatua ya Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (Nemc) kuyafunga machinjio ya Ukonga.
Nemc imeyafunga machinjio hayo yaliyoko eneo la Ukonga Mazizini katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, baada ya kubaini kuwa yanaendesha shughuli zake katika mazingira machafu yanayohatarisha afya za walaji wa nyama.
Machinjio hayo ambayo ng’ombe kati ya 350 hadi 500 huchinjiwa hapo, yamefungwa baada ya maofisa wa Nemc wakiongozwa na Afisa Mwandamizi Mkuu wa baraza hilo, Lucy Lugusha, kufanya ziara ya ukaguzi wa kushtukiza katika eneo hilo.
Maofisa hao walifika katika machinjio hayo jana majira ya asubuhi  na kumkuta Afisa Mfawidhi wa Machinjio ya Ukonga, Pradisius Mbita, ambaye pia ni mtumishi wa Manispaa ya Ilala akiwa katika ofisi za wamiliki wa machinjio hayo.
Kabla ya kuanza ukaguzi, Mbita aliulizwa na maofisa wa Nemc kuna mahusiano gani kati ya Manispaa ya Ilala na machinjio hayo na kueleza kuwa manispaa imekuwa ikikusanya ushuru tu na kwamba kuna watumishi ambao wameteuliwa rasmi kufanya kazi katika machinjio hayo.
Mbita alisema watumishi wa manispaa ambao wanafanya kazi katika machinjio hayo yaliyoanzishwa tangu mwaka 1972, ni pamoja na yeye mwenyewe (Mbita) kama mkaguzi wa nyama, afisa afya, mhasibu na mlinzi.
Alipoulizwa kama machinjio hayo yana leseni, Mbita alisema manispaa haina uhakika kama kuna leseni yoyote iliyokatwa kwa ajili ya kuendesha machinjio hayo.
Baada ya maofisa hao wa Nemc kuendelea kumhoji Mbita, alijitetea kuwa masuala mengine ni ya ndani zaidi, hivyo ni bora akamwita mmoja wa wamiliki wa machinjio hayo ayajibu.
Baada ya nusu saa, mmoja wamiliki wa machinjio hayo, Philemon Bereko, aliwasili eneo hilo na kueleza kuwa machinjio hayo yanamilikiwa na watu watatu ambao ni Philemon Bilia, Anthony Bilia na yeye mwenyewe (Bereko).
Bereko ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa wachinja Nyama, alisema kama ilivyo kwa Nemc, nao wamekuwa wakipata malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu mazingira machafu ya machinjio hayo.
Alisema Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala alishawahi kufika katika machinjio hayo baada ya kupata malalamiko kutoka kwa wananchi na aliahidi kuwa halmashauri itatoa fedha zinazotokana na ushuru unaotozwa katika machinjio hayo kwa ajili ya kusaidia kuboresha mazingira.
Bereko alisema tangu Mkurugenzi wa Manispaa alipondolewa, ahadi hiyo imekwama kutekelezwa badala yake halmashauri hiyo imekuwa ikiendelea kukusanya ushuru wake wa Sh. 2,500 kwa kila ng’ombe mmoja anayechinjwa katika machinjio hayo.
“Halmashauri wameweka hadi mhasibu wao hapa, kila ng’ombe anayechinjwa ushuru unaotozwa ni Sh. 2,000 na Sh. 500 ni za mkaguzi wa nyama ambaye anatoka halmashauri, mazingira haya wanayaona na mvua ikinyesha hali inakuwa mbaya sana,” alisema Bereko.
Hata hivyo, alipoulizwa inakuwaje machinjio hayo yaendeshwe na watu binafsi halafu halmashauri ichangie kuyaboresha, alisema hayo ni katika makubaliano yao na kwamba kinachomsikitisha ni hatua ya halmashauri kuweka mhasibu katika machinjio hayo wakati katika maeneo mengine hakuna utaratibu kama huo.
Baada ya kikao hicho, maofisa wa Nemc walianza ukaguzi wa machinjio hayo na kujionea hali ya kutisha ya uchafu wa mazingira katika eneo hilo ambayo yanahatarisha usalama kwa mlaji wa nyama inayochinjwa.
Miongoni mwa mambo yaliyobainika ni mamia ya tani za kinyesi cha ng’ombe ambacho kimerundikana, mifereji ya kupitishia maji yaliyochanganyika na damu kutitirika katika mtaro wa maji unaounganishwa katika mto ambao unaingiza maji kwenye Bahari ya Hindi na kupita kando kando ya makazi ya watu.
Pia mazizi ya kuhifadhi ng’ombe kabla hazijachinjwa yamejaa maji machafu yaliyochanganyika na kinyesi kiasi kwamba ng’ombe akiwa humo huzama miguu.
Maofisa wa Nemc walipofika eneo la machinjio na kufanya ukaguzi saa 5:45 asubuhi, hapakuwapo na nyama, lakini nzi na funza walionekana kutokana kukithiri kwa uchafu.
Baada ya kujionea hali hiyo, Afisa Mwandamizi Mkuu wa Nemc, Lugusha, alitoa agizo la kusitisha shughuli za uchinjaji nyama katika machinjio hayo hadi hapo mazingira ya usafi yatakapoboreshwa.
“Mchana wa leo (jana), tutakuletea barua rasmi ya kukutaka usitishe shughuli za kuchinja nyama katika machinjio haya na nakala tutapeleka Halmashauri ya Manispaa ya Ilala,” alisema Lugusha.
Hata hivyo, Bereko alijitetea kwamba apewe muda wa mwezi mmoja au wiki moja arekebishe mazingira hayo, lakini ombi lake lilikataliwa na maofisa wa Nemc ambao walimweleza kuwa aanze kazi ya kuboresha mazingira na akimaliza ndipo ataruhusiwa kuendelea na uchinjaji.

No comments: