Wednesday, April 24, 2013

Maalim aonya wanaouza miche ya karafuu nje

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad ameonya kuwa Serikali haitavumilia na itawachukulia hatua za kisheria watu watakaobainika kukata miti na kusafirisha miche ya miti ya mikarafuu nje ya nchi kinyume cha sheria.

Maalim Seif alitoa onyo hilo Bwagamoyo Mtambwe, Mkoa wa Kaskazini Pemba, alipokuwa akizindua kampeni ya upandaji miti Zanzibar.

Alisema baadhi ya watu wamekuwa na tabia ya kukata miti ovyo, ikiwamo mikarafuu na wapo ambao wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya kuisafirisha miche ya mikarafuu nje ya nchi, ikiwamo Kenya.

Alisema tabia ya kukata miti kiholela ni hatari kwa mazingira na husababisha athari kubwa kiuchumi, lakini vitendo vya kusafirisha nje ya nchi miche ya mikarafuu kinaweza kushusha hadhi ya Zanzibar iliyojijengea kwa miaka mingi kuwa mzalishaji mkuu wa karafuu.

Alieleza kuwa karafuu ni alama ya Zanzibar, ambayo imeifanya ijuilikane duniani kote kuwa ni visiwa vya viungo, lakini baada ya watu kuona thamani ya zao hilo ilishuka katika miaka iliyopita walilidharau na kuikata miti hiyo kwa ajili ya kujengea nyumba, kuni na makaa.
Alisema katika karne iliyopita zao la karafuu lilithaminiwa sana na wazee waliliotesha kwa wingi hadi kufikia hatua Zanzibar ikizalisha tani zaidi ya 35, 000.

No comments: