Friday, April 25, 2014

Siku ya Albino Mei 4

CHAMA cha Albino Tanzania (TAS) kimesema maadhimisho ya tisa ya Siku ya Albino kitaifa yatafanyika Mei 4 na itakuwa siku ya kudai haki ya afya na uhai.
Pia kimesema kutokutekelezwa kwa haki hiyo ni sawa na kutokukidhi haki ya kuishi na kubagua sehemu ya jamii.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam juzi, Ofisa Habari wa TAS, Josephat Torner, alisema maadhimisho hayo yanalenga kuongeza ufahamu wa jamii juu ya masuala ya ualbino na utekelezaji wa mkataba wa kimataifa wa haki za watu wenye ulemavu.
“Mkataba huu wa kimataifa wa haki za watu wenye ulemavu nchi yetu imekwishausaini na kuridhia, utekelezaji wake upo katika hatua mbalimbali, hivyo maadhimisho haya yataongeza ufahamu kwa jamii kuhusu mikataba hii,” alisema Torner.
Alisema maadhimisho hayo yatawashirikisha wadau wa ualbino toka mataifa mbalimbali ulimwenguni ikiwa ni pamoja na nchi za Afrika Mashariki na Kusini, Marekani na Ulaya.
“Wageni hawa watashiriki katika mkutano wa siku moja wa kimataifa utakaozungumzia masuala ya albino na changamoto zinazowakabili, pia matarajio ya mkutano huu ni kupata sauti pana itakayotangaza siku hii kimataifa,” alisema.
Alitoa rai kwa watu wote wenye ualbino, wazazi, walezi pamoja na wadau mbalimbali kwa ujumla kujitokeza kwa wingi katika maadhimisho hayo.

No comments: