Friday, April 25, 2014

Jukata: Rais Kikwete si refa mzuri

JUKWAA la Katiba Tanzania (Jukata) limesema Rais Jakaya Kikwete, amepoteza urefa aliouvaa wakati anaanzisha mchakato wa kupata Katiba na kuvaa jezi ya chama kimoja. Jukata wameeleza kuwa kutokana na hali hiyo Bunge la Katiba limepata mpasuko huku Mwenyekiti wake, Samuel Sitta, akipwaya kiuamuzi kutokana na kutokemea mivutano na uhalalishaji wa kuvunja kanuni.
Aidha, Jukata wamemuomba Jaji Mkuu mstaafu, Barnabas Samatta na Patrice Lumumba, kutoka Kenya kusaidia kusimamia unasuaji wa mchakato wa katiba unaoonekana kukwama baada ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kususia.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Jukata, Deus Kibamba, alisema bila upatanisho mchakato huo utakwama na kuongeza kuwa kwa sasa Kikwete amepoteza uwezo wa kusuluhisha.
Kibamba alisema baada ya UKAWA kutoka nje ya Bunge na kugoma kurudi kumeleta pigo katika mchakato wa katiba na kutia dosari iliyosababisha matusi na mivutano.
“Rais lazima atambue kuwa si rais wa CCM pekee bali ni rais wa watu wote, hivyo kujionyesha kuegemea upande mmoja kunaleta mpasuko kwa taifa… rais alipaswa kujizuia katika kutamka misimamo yake ya nini anataka kwenye Katiba,” alisema Kibamba.
Katika tathmini iliyofanywa na jukwaa hilo imebaini kuwa kuingia moja kwa moja kwa wabunge na wawakilishi kwenye Bunge maalumu la Katiba ndiyo sababu ya mchakato huo kuwa hapo ulipo.
Alisema tathmini yao imebaini kuwapo na migongano ya kimasilahi kuhusu wanasiasa na masilahi yao ya vyeo na mapato.
“Ukiisoma rasimu ya pili ya katiba inaeleza kuwa kutakuwa na wabunge 75, sasa piga hesabu kutoka 360 hadi 75 hapo lazima viongozi wapate hofu,” alisisitiza.
Pia alisema sheria ya mabadiliko ya katiba sura ya 83 ya sheria za Tanzania imempa rais madaraka kwa hatua zote za mchakato huo.
Alisema mivutano iliyopo sasa imesababishwa na kupindishwa kwa sheria wakati wa ufunguzi wa bunge hilo hali iliyosababisha kuchochea kuligawa kivyama, kimisimamo na kiitikadi.
Aidha, alisema kuwa kitendo cha viongozi wa dini kuegemea pande kunaendeleza mivurugano na kuongeza kuwa viongozi hao wanapaswa kuongoza toba ya taifa na si kuongoza kulipasua taifa kwa kauli zao.
“Tusahihishe makosa katika mchakato wa katiba na hasa sheria ya mabadiliko ya katiba ili kuweka sawa mambo yenye utata yahusuyo elimu ya uraia, demokrasia ya mijadala na mamlaka ya wananchi katika mchakato huo,” alisema.
Kibamba aliongeza kuwa tangu kuanza kwa mchakato wa katiba Desemba 31, 2010 hadi jana bado imeshindikana kupatikana katiba mpya ambayo ilipangwa kuzinduliwa leo sambamba na maadhimisho ya miaka 50 ya  Muungano.

No comments: