Friday, April 25, 2014

Miradi ya TASAF yawainua wakazi Chamwino

WAKAZI wa Kijiji cha Ndogowe na Ng’ambaku katika Wilaya ya Chamwino, mkoani Dodoma, wamesema miradi inayosimamiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) imekuwa mkombozi wa kuwaondolea umaskini.
Aidha, walieleza miradi hiyo imewafanya kuondokana na hali ya kuwa ombaomba na badala yake wameweza kujenga utamaduni wa kujitegemea.
Wakazi hao walibainisha hayo kwa nyakati tofauti walipozungumza na Tanzania Daima katika mahojiano maalumu juu ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa na TASAF kwa lengo la kuzinusuru familia lengwa katika hali ya umaskini.
Mmoja wa wanufaika wa mradi huo, Axa Mporo (78), ambaye ni mjane alisema kabla ya Tasaf kumuingiza katika mpango wa miradi ya kunusuru kaya maskini alikuwa ombaomba wa kutupwa.
Alisema alikuwa hawezi kufanya jambo lolote na wakati huo alikuwa ni mtu wa kuombaomba, kwani hakuwa na uwezo hata wa kununua chumvi.
“Nilikuwa siwezi kufanya jambo lolote na nilikuwa maskini kweli kweli, mume wangu alikuwa ni kibarua, lakini zaidi mimi nilikuwa siwezi kununua  hata chumvi. Mume wangu alipofariki dunia maisha ndiyo yakazidi kuwa mabaya,” alisema.
Alisema baada ya kuingizwa katika mradi huo na kupatiwa elimu na kisha kupatiwa fedha alinunua shamba kwa ajili ya kilimo na kwamba kwa sasa anaweza kupata chakula na hata huduma za matibabu.
“Tasaf wamekuwa mkombozi wa maisha yangu, kwani sasa napendeza tofauti na awali wakati nikiombaomba,” alisema Axa.
Katibu wa mpango wa uwahilishaji fedha kwa kunusuru kaya maskini, Mussa Mwendi, alisema miradi ya kunusuru kaya maskini ilianza mwaka 2010 ikiwa na walengwa 162 na kwa sasa wapo walengwa 276.
Alisema tangu kuanza kwa miradi ya maendeleo hadi sasa jumla ya sh milioni 59.3 zimewafikia familia lengwa ambazo ni maskini.
Mkurugenzi Mratibu wa Tasaf, Alphonce Kyaliga, aliwataka wanavikundi ambao ni kaya lengwa kuhakikisha wanajihusisha katika miradi ya maendeleo kwa lengo la kujinusuru katika dimbwi la umaskini.

No comments: