Friday, April 25, 2014

Mil. 115/- kukabili ukimwi Kilolo

HALMASHAURI ya Wilaya ya Kilolo, mkoani Iringa imetenga sh milioni 115.5 kwa ajili ya kutekeleza pambano dhidi ya ugonjwa wa ukimwi kwa mwaka wa fedha 2014/2015.
Mwenyekiti wa Kamati ya Wilaya wa Kudhibiti Ukimwi, Peter Mbosa, alieleza hayo alipokuwa akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo katika kikao cha kawaida cha baraza la madiwani kilichoketi hivi karibuni.
Alisema fedha hizo zinatokana na  chanzo cha mapato mengine na msaada kutoka  Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) kwa lengo la kutekeleza shughuli mbalimbali za mapambano dhidi ya ukimwi.
Mbosa alisema sh milioni 3.3 zitatumika katika kutoa huduma za dawa za kupunguza makali ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) katika vijiji vya Mawambala na Ipalamwa.
Wakichangia hoja wakati wa kujadili matumizi sahihi ya fedha hizo, baadhi ya madiwani walisema huduma za upatikanaji wa dawa za kupunguza makali ya VVU ziwafikie walengwa kwa wakati na zitolewe katika vituo vyote vya afya.
Pia walisema kuna umuhimu wa kuhamasisha wananchi kwenda kupima afya zao na kuishi maisha ya uaminifu ili kupunguza maambukizi mapya ya VVU.

No comments: