Friday, April 25, 2014

Macho yote vipaji vipya Stars leo

WAKATI timu ya soka ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ ikishuka Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo kucheza pambano la kirafiki la kimataifa dhidi ya Burundi, Kocha wa muda wa Stars, Salum Mayanga, ameahidi kuwaanzisha kikosi cha kwanza nyota wawili au watatu ‘yoso’ waliozalishwa na programu ya maboresho ya Stars. Stars inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager, inawaalika Burundi ‘Itamba Mu Rugamba’ ikiwa ni sehemu ya Sherehe za Miaka 50 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na maandalizi ya awali kwa mechi za kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON 2015), zinazotarajiwa kufanyika mwakani nchini Morocco.
Wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, makocha na manahodha wa timu zote walitamba kuwa tayari kuonyesha burudani ya uhakika kuzipamba sherehe za Muungano, huku Mayanga akisema atawapa nafasi yoso wawili au watatu, kisha kuwaongeza zaidi katika mabadiliko yake mchezoni.
“Najua Watanzania watataka kuona matunda ya kambi ya mafunzo ya mpango wa maboresho ya Taifa Stars, ingawa hiyo haiwezi kunifanya nikurupuke na kuwajaza kikosini, kwani bado ni wachanga na wanahitaji muda. Nitawaanzisha wachache, kisha wataongezeka kupitia ‘sub’ nitakazofanya,” alisema Mayanga.
Kwa upande wake, Nahodha wa Stars, Aggrey Morris, aliahidi kikosi chake kutowaangusha Watanzania katika sherehe hizo na kwamba, nyota wake wako tayari kwa changamoto iliyo mbele yao, huku akiwataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kuwapa sapoti.
Morris anayekipiga Azam FC, aliwataka mashabiki wa soka na Watanzania kuwa tayari kwa matokeo yoyote, kwani soka lina aina tatu za matokeo, ambayo ni kushinda, kufungwa ama sare, hasa ukizingatia kikosi chake kinajumuisha nyota waliozalishwa na programu maalumu ya maboresho ya Stars.
“Watanzania wanapaswa kuwapa muda wa kuiva kisoka vijana hawa, kabla ya kutarajia makubwa zaidi kutoka kwao. Naamini tuna kila sababu ya kushinda mechi hii, ambayo kwangu mimi ni kipimo sahihi kabisa kuelekea AFCON 2015,” alisisitiza Morris.
Kwa upande wake, Kocha wa Burundi, Niyungeko Alain Olivier, alisema vijana wake wana ari kubwa ya kushinda mechi hiyo bila kujali matokeo yaliyopita baina ya nchi hizo, huku akielekeza matumaini yake kwa watikisa nyavu wawili wanaosakata kabumbu nchini, Amisi Tambwe na Didier Kavumbagu.
Kavumbagu anayekipiga Yanga na nahodha wa Burundi, aliambatana na kinara wa mabao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Tambwe, katika mkutano huo. Wakali hao wanampa matumaini makubwa Olivier, ingawa hakutaka kubainisha hilo katika mkutano huo.
Nahodha huyo wa Burundi aliahidi burudani kwa kila shabiki atakayehudhuria mechi hiyo, huku akitaka uwepo wa ‘fair play’ kutokana na umuhimu wa mechi kwa sherehe za Muungano, lakini pia kudumisha undugu na ushirikiano baina ya Tanzania na Burundi.
Viingilio katika mechi hiyo inayotarajiwa kuchezeshwa na mwamuzi Mkenya, Anthony Ogwayo, mwenye beji ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), vitakuwa sh 5,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, bluu na kijani. Katika jukwaa la VIP A, kiingilio kitakuwa sh 20,000, wakati VIP B na C ni sh 10,000.

No comments: