Friday, April 25, 2014

JK: Atakayechezea Muungano kukiona

RAIS Jakaya Kikwete ameonya kuwa mtu atakayechezea Muungano atakiona cha mtema kuni. Rais Kikwete alitoa kauli hiyo jana wakati akilihutubia taifa kwenye hafla ya kuwapongeza vijana wa Umoja wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), waliozunguka nchini nzima kuunga mkono Muungano wa serikali mbili.
Rais Kikwete alitumia mkutano huo kulihutubia taifa kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano inayoadhimishwa leo.
Rais Kikwete ambaye ametoa hotuba hiyo katika Ukumbi wa PTA jijini Dar es Salaam, alisema kuwa leo si siku ya kuzungumza bali ni siku ya jeshi kuonyesha umahili wao.
“Sherehe za kesho ni sherehe za jeshi ambao wamepania kuonyesha watakavyoulinda Muungano na atakayeuchezea atakiona cha mtema kuni,” alisema Rais Kikwete.
Bila kutaja majina, Rais Kikwete alisema kuna kundi la watu ambao viongozi wake wanatumia milango ya VIP kusafiri, linataka kuvunja Muungano na kusisitiza kwamba serikali itapambana kwa gharama yoyote ile kuulinda Muungano.
Ingawa Rais Kikwete hakutaja majina, lakini alikuwa akiwalenga viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ambao pamoja na wajumbe wao wameamua kususia vikao  vya Bunge Maalumu la Katiba.
Viongozi hao, Freeman Mbowe, Profesa Ibrahim Lipumba, James Mbatia na wajumbe wao, wametoka bungeni kwa madai ya kutoridhishwa na namna Bunge hilo linavyoendeshwa, huku baadhi ya mawaziri wa serikali wakiingia ndani ya makanisa kuwatisha wananchi kwamba serikali tatu zikipitishwa jeshi litapindua nchi.
UKAWA wanaeleza kuwa wametoka baada ya kuona kuwa CCM imeamua kujadili rasimu yao badala ya ile iliyotokana na maoni ya wananchi yaliyokusanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba.
Viongozi wa UKAWA, wamekuwa wakieleza bayana kwamba hakuna mwenye nia ya kuvunja Muungano, lakini wajumbe wanaotokana na CCM wamekuwa wakidai kwamba UKAWA wanataka kuvunja Muungano.
Rais Kikwete alitetea dhamira yake ya kuanzisha mchakato wa Katiba kwamba ilikuwa na  nia ya kujadili kwa uwazi na mapana yale yanayotakiwa yaingizwe au kuondolewa ndani ya Katiba ili kuondoa kero za Muungano.
“Niliwaambia siku ya kuzindua Bunge kuwa wajumbe watumie fursa hii kutuletea katiba nzuri, fursa ambayo itaondoa matatizo ya Muungano.
“Lazima nikiri kwamba sikufurahishwa hata kidogo na baadhi ya wajumbe kususia vikao, eti wanazunguka kwenda kushitaki kwa wananchi, sijui wanakwenda wapi na kumshitaki nani, huko nje waendako siko, wakati wake bado. Nawasihi warudi bungeni, hawawatendei haki wananchi wao,” alisema Kikwete.
Rais Kikwete aliungana na viongozi wengine wanaowataka UKAWA warejee bungeni badala ya kubaki nje ili kufanikisha upatikanaji wa Katiba.
Alisema  wajumbe wa Bunge la Katiba wana matatizo na matatizo yao ni ya mahusiano na kamwe hawawezi kupata jawabu kwa wananchi wanakokwenda kwani watakachofanya wananchi hao ni kusikitika pamoja nao tu.
Alisema majawabu ya matatizo yao hayawezi kutatuliwa kwa wananchi bali ndani ya Bunge ambalo wameliwekea kanuni ya namna ya kumaliza matatizo yao.
Rais Kikwete pia alielezea lugha iliyokuwa ikitumiwa na wajumbe hao kwamba si nzuri kwani haina staha, hivyo aliwataka wajue kuwa haiba na vitendo vyao viendane na hadhi yao.
Kuhusu hati ya Muungano ambayo ilikuwa gumzo ndani ya Bunge, Rais Kikwete alisema aliamua kuitoa hati hiyo hadharani baada ya kuona Bunge linataka kupoteza mwelekeo.
“Nilipoona mjadala unapoteza mwelekeo, nikamwita Katibu Mkuu Kiongozi, nikamwambia itoe hadharani, tumeitoa, kelele zikaanza kwamba saini ya Karume imeghushiwa,” alisema Rais Kikwete.

No comments: