Sunday, April 27, 2014

MWANZA WATAKIWA KUDUMISHA MUUNGANO

 
Wananchi mkoani Mwanza,  wametakiwa kudumisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ili kuwaenzi waasisi wa taifa hili hayati Amani Karume na Mwl Julias kambarage Nyerere kwa kutenda mema waliyoyafanya.
 
Kauli hiyo ilitolewa na mgeni rasmi mkuu wa wilaya ya Ilemela Amina Masenza ambaye alikuwa akimwaakilisha mkuu waa mkoa wa Mwanza Eng Evarist Ndikillo alipokuwa akiwahutubia mamia ya watu  kwenye kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya muungano ambayo kimkoa yalifanyika katika  viwanja vya shule ya msingi Sengerema kata ya Nyampulukano wilayani Sengerema Mkoani Mwanza.
 
Bi Masenza alisema kuwa wananchi wote kwa ujumla wanatakiwa kudumisha muungano  wa Tanganyika na Zanzibar kwa  amani na utulivu na kuwaepuka wanasiasa wenye uchu wa madaraka na wapotoshaji ambao wanataka kuvuruga amani ya nchi  ya Tanzania kwa maslahi yao binafsi .
 
“Kuna kila sababu ya kuwakumbuka viongozi wetu hawa wawili Karume na Nyerere  kwani leo hii tunaadhimishaa miaka 50 ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa wao kutuonganisha, tumekuwa tukifanya biashara kwa pamoja na kuoleana” alisema Bi Masenza
 
Aidha aliongeza kuwa wananchi waliowengi walizoea serikali mbili ambapo muungano utakapovunjika wananchi wengine hawana pa kukimbilia.
 
Pia katika hotuba yake alikemea ubaguzi wa rangi na ukabila na kuwaasa wana Mwanza kudumisha muungano na kuonyesha mbegu bora walizopanda ambapo changamoto za muungano ni fursa na sio kuvuruga amani ya nchi.
 
“ Hatma ya muungano wetu ipo mikononi mwetu…… tuimarishe muungano wetu..” alisema Bi Masenza.
Na Dotto Mgaza- Sengerema

No comments: