Friday, October 25, 2013
Thursday, October 17, 2013
SHEIKH JONGO ABEBESHA WAISLAMU ZIGO
Kadhi wa
Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Hamid Jongo, amepinga madai, ambayo yamekuwa
yakitolewa na baadhi ya watu kwamba, ndani ya serikali kuna mtandao wa
Wakristo, ambao wanawachukia Waislamu na kusema wenye matatizo ni Waislamu
wenyewe.
Sheikh
Jongo, ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza la Ulamaa la Baraza Kuu la Waislamu
Tanzania (Bakwata), alisema hayo wakati akihutubia katika sherehe za Baraza la
Idi el-Hajj, zilizofanyika katika Msikiti wa Al-Farouq, Makao Makuu ya Bakwata,
Kinondoni, jijini Dar es Salaam jana.
Alisema kwa
mujibu wa utafiti alioufanya hakuna mtandao wa Wakristo ndani ya serikali, ila
mtandao unaweza kuwapo ndani ya Wakristo wenyewe kama ambavyo unaweza pia
kuwapo ndani ya Waislamu na si serikalini.
Sheikh Jongo
alisema kinyume cha madai hayo, ukweli uliopo ni kwamba, Waislamu wenyewe ndiyo
wenye matatizo, ambao hawana nidhamu, utaratibu na uongozi kiasi ambacho kila
mmoja amekuwa mwamuzi wa mambo yanayohusu Uislamu.
Alisema
inashangaza kuona leo Mufti anatangaza kuwa kesho ndiyo Idi, baadhi ya Waislamu
wanasema leo.
“Wakristo, serikali, CCM hawana matatizo hata
kidogo. Wenye matatizo ni sisi wenyewe
Waislamu,” alisema Sheikh Jongo.
Alisema
matajiri wengi nchini ni Waislamu, lakini Waislamu wanashindwa kuwaendea
kuwaomba wawasaidie mambo ya kimaendeleo, kama vile elimu, badala yake
wanawaendea kwa ajili ya kuomba misaada ili wakaoe, jambo ambalo alisema
matajiri ‘wamelishtukia’.
“Tusiwadhulumu Wakristo. Kama wanaimarisha
dini yao na sisi tuimarishe dini yetu. Chuo Kikuu Morogoro katupa Mkapa
Mkristo. Lakini sisi wenyewe hata chumba kimoja hatuna,” alisema Sheikh Jongo.
Alisema
Waislamu wanamiliki maghala mengi, ambayo wanaweza kuyatumia kuanzisha vyuo
vikuu na kuhoji: “Kwanini hatuanzishi Chuo Kikuu?”
Sheikh Jongo alisema iwapo Waislamu wenyewe
watatumia rasilimali walizonazo kuanzisha Chuo Kikuu kisha serikali ikawanyima,
wataandamana na yeye ndiye atakayeongoza hayo maandamano.
Alisema
maadui wa Waislamu waliotajwa na Kur’ani Tukufu ni shetani na Mayahudi na
kuhoji: “Umepata wapi Wakristo ni maadui wa Waislamu?”
“Uislamu huu
unaofanywa na wapigadebe siyo ule aliokuja nao Mtume S.A.W. Uislamu wa Mtume ni
amani na utulivu,” alisema Sheikh Jongo.
Awali,
akiwasilisha salamu za Bakwata katika sherehe hizo, Katibu Mkuu wa Bakwata,
Ustadh Suleiman Lolila, aliiomba serikali kusitisha utekelezaji wa kanuni mpya
za mtihani za mwaka 2013, ambazo zimeyapanga baadhi ya masomo, yakiwamo ya dini
zote katika kundi la hiari.
Alisema kwa
mujibu wa kanuni hizo mpya za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, masomo ya
dini zote, lugha ya Kiarabu, Kifaransa na Kompyuta, hayatatumika katika
kutunuku ufaulu wa wanafunzi, hasa katika kumpangia daraja.
“Tunaomba
Wizara ya Elimu isitishe utekelezaji wa zoezi hili kama ilivyoainishwa katika
Examination Regulations (kanuni za mtihani) ya mwaka 2013 hadi hapo mazungumzo
kati ya wakuu wa taasisi za dini zote zenye shule na Wizara ya Elimu
yatakapofanyika kwa manufaa ya taifa letu.
Tunaiomba
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi iharakishe kuitisha kikao hicho na kufikia mwafaka kwa
mustakabali mwema wa taifa letu,” alisema Ustadh Lolila.
Alisema dini
ndiyo inayowajenga watoto na raia wa kesho kimaadili, hivyo wangetegemea
serikali kuweka mkazo katika masomo hayo ili yatahiniwe na kumpa mwanafunzi
ufaulu wa kusonga mbele na hapo hapo kumsaidia kujenga maadili mema ya Taifa
kwa vijana.
Alisema pia
wanafunzi wa shule za msingi kwa kujua kwamba, masomo hayo hayana tija,
wakifika sekondari, ni rahisi kupuuzia kusoma masomo ya dini na kwamba, tatizo
la maadili litaongezeka katika jamii endapo masomo ya dini hayatatahiniwa.
Alisema pia
vyuo vikuu vya ualimu nchini, kama vile Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro, Chuo
Kikuu cha Zanzibar na vyuo kadhaa vya ualimu vyenye mitaala hiyo vitakosa
wanafunzi.
Alisema
vilevile, vyuo vingi vitaathirika na idadi ya Watanzania wanaokwenda vyuo vikuu
kupungua sana.
Alisema wapo
pia Watanzania wanaojiunga na vyuo vya kimataifa vinavyotumia mchepuo wa masomo
ya dini kama Chuo Kikuu cha Makerere, vyuo vikuu vya Sudan na Misri na kwingine
ulimwenguni kote, wataathirika vibaya na uamuzi huo wa serikali.
Akijibu hilo, Waziri wa Maji, ambaye alikuwa
mgeni rasmi katika sherehe hizo, Profesa Jumanne Maghembe, alisema amelipokea
na kwamba, atalifikisha kwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru
Kawambwa, haraka iwezekanvyo na kwamba, suala waliloomba litapatiwa ufumbuzi.
Hata hivyo,
alisema mchango wa Waislamu katika elimu haulingani na uwezo na wingi walionao,
hivyo akawaomba waisaidie serikali kuandaa wataalamu na vijana kutoa mafundisho
ya dini ya Kiislamu.
Naye Kaimu
Mufti wa Tanzania, Sheikh Ismail Habib Makusanya, alisema tofauti na huko
nyuma, hivi sasa kuna dalili za kuvunjika amani na utulivu kunakofanywa na
baadhi ya watu nchini, hivyo akaishauri serikali kuwa wakali ili kuwadhibiti
watu wa aina hiyo.
Chanzo:Nipashe
Tuesday, October 15, 2013
SWALA YA IDD YAFANYIKA LEO MJINI IRINGA KATIKA UWANJA WA MWEMBETOGWA
Sehemu ya waumini wa dini ya kiisalam wakiwa katika uwanja wa mwembetogwa wakisubiri ibada ya swala ya idd
Waumini wa dini ya kiislamu wakitoka baada ya swala ya idd iliyosaliwa katika uwanja wa mwembetogwa manispaa ya ringa
Sehemu ya akina mama wakitoka kutekeleza ibada ya swala ya idd leo iliyosaliwa manispaa ya iringa
Waumini wa dini ya kiislamu wakitoka baada ya swala ya idd iliyosaliwa katika uwanja wa mwembetogwa manispaa ya ringa
Sehemu ya akina mama wakitoka kutekeleza ibada ya swala ya idd leo iliyosaliwa manispaa ya iringa
Tuesday, September 17, 2013
MAKALA MAALUM-IBADA TUKUFU YA HIJJA
Ibada ya Hijjah ndio
inayozikamilisha nguzo tano za Uislamu, amesema Allah Mola Mwenyezi: “...NA
ALLAH AMEWAWAJIBISHIA WATU WAFANYE HIJJAH KATIKA NYUMBA HIYO; YULE AWEZAYE
KUFUNGA SAFARI KWENDA HUKO...” [3:97] Na akasema tena: “NA (tukamwambia):
UTANGAZE KWA WATU KHABARI ZA HIJJAH, WATAKUJIA (wengine) KWA MIGUU NA (wengine)
JUU YA KILA MNYAMA ALIYECHOKA (kwa machofu ya njiani) WAKIJA KUTOKA KATIKA KILA
NJIA YA MBALI. ILI WASHUHUDIE MANUFAA YAO NA (ili wakithirishe) KULITAJA JINA
LA ALLAH KATIKA SIKU ZINAZOJULIKANA...” [22:27-28] Imepokewa kutoka kwa Abu
Hurayrah-Allah amuwiye radhi-amesema-Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-amesema: “Enyi watu! Hakika Allah amekufaradhishieni Hijjah, basi
hijini (nendeni Hijjah). Atakayehiji kwa ajili tu (ya kutaka radhi za) Allah na
asiseme maneno machafu wala asifanye vitendo vichafu, atatoka katika madhambi
yake kama siku aliyozaliwa na mama yake. Na Umrah moja mpaka nyingine ni kafara
ya madhambi ya kipindi kilicho baina ya (Umrah) mbili hizo na Hijjah yenye
kukubaliwa haina jazaa (malipo) ila pepo”. Bukhaariy & Muslim-Allah
awarehemu.
Katika mithili ya masiku kama
haya kila mwaka, macho, masikio na nyoyo za waislamu ulimwenguni kote
huelekezwa nchini Saudi Arabia. Khususan katika mji Mtakatifu wa Makkah; mahala
ambapo ipo nyumba takatifu na kongwe ya Allah, nyumba inayotajwa na kauli
tukufu ya Allah: “KWA YAKINI NYUMBA YA KWANZA ILIYOWEKWA KWA AJILI YA WATU
(kufanya ibada) NI ILE ILIYOKO MAKKAH, YENYE BARAKA NA UONGOZI KWA AJILI YA
WALIMWENGU WOTE. HUMO MNA ISHARA ZILIZO WAZI (za kuonyesha utukufu wake na ukongwe
wake. Miongoni mwa hizo ni) MAHALA ALIPOKUWA AKISIMAMA IBRAHIMU, NA ANAYEINGIA
(Haram) ANAKUWA KATIKA SALAMA...” [3:96-97]
Waja wa Allah huuitikia wito wa
Mola wao katika masiku haya kwa kufunga safari kutoka pande mbalimbali za dunia
kuielekea nyumba hii tukufu ya Allah. Huenda huko kwa ajili tu ya kuitekeleza
ibada ya Hijah ambayo ni nguzo ya tano ya Uislamu; dini na mfumo wao sahihi wa
maisha. Ibada hii tukufu huwakutanisha pamoja ndugu wa imani wa mataifa, lugha,
hadhi na rangi mbalimbali. Huu ni mkutano na mkusanyiko usio na mithali yake
katika ulimwengu huu, ulimwenguni kote haujapata na wala hautapata kutokea
mkusanyiko unaowakusanya watu wengi na wa mataifa mengi kama huu wa Hijjah.
Kutokana na utukufu na umuhimu wa ibada hii tukufu ya Hijjah, Website yako
(WEBSITE UISLAMU) inajifakharisha kwa mara nyingine tena kuifanyia kazi kauli
tukufu ya Allah: “...NA SAIDIANENI KATIKA WEMA NA TAQWA, WALA MSISAIDIANE
KATIKA MADHAMBI NA UADUI”. [5:2] Ili kukusaidia wewe ndugu mpenzi Hajji
kuitekeleza kauli ya Allah Mola Mlezi wako: “NA TIMIZENI HIJJAH NA UMRAH KWA
AJILI YA ALLAH...” [2:196] Website yako inakuletea maelezo haya mukhtasari
inayopenda kuyaita (MUONGOZO WA HIJJAH NA UMRAH) huku ikiamini kwa yakini
kwamba inachangia katika suala zima la kusaidiana katika WEMA na TAQWA. Ni
matumaini ya Website Uislamu kwamba utaupokea muongozo huu kwa mikono miwili na
kupupia kuusoma kwa nia ya kujifunza, kujua na kuutumia katika kipindi chote
cha kuitekeleza kwako ibada hii tukufu. Kadhalika ni matarajio ya Website
Uislamu kuwa muongozo huu utakupa msaada mkubwa utakaokuwezesha kuitekeleza
ibada hii kwa UJUZI WA KWELI. Website
Uislamu inawatakia mahujaji wote Hijjah njema iliyotakasika kwa ajili ya Allah.
Haya sasa karibu katika MUONGOZO WA HIJJAH NA UMRAH, kwa jina la Allah na kwa
kuutaraji mno msaada na taufiq yake tunaanza kwa:
- USIA MUHIMU:
Enyi mahujaji, Website yenu (WEBSITE
UISLAMU) inapenda kuitumia fursa hii adhimu kumuhimidi Allah aliyekuwafikisheni
kwenda kuhiji katika nyumba yake tukufu. Kama alivyokuwafikisheni kuhiji
tunamuomba akutakabalieni ibada yenu hii na baki ya amali nzenu njema, Aamiyn!
Ili kuhakikisha kuwa unafuzu katika kuitekeleza ibada hii, tunapenda kwa
mapenzi ya Allah kukupa wasia muhimu kama ifuatavyo:
a) Kumbukeni
kwamba nyinyi kama mahujaji mumo katika safari tukufu yenye baraka tele za
Allah. Pia mumo katika Hijrah; mnaiacha miji yenu, watu wenu na shughuli zenu
kwa ajili tu ya kuuitika wito wa Mola wenu. Fahamuni-Allah akurehemuni-kwamba
safari yenu hii ina ujira adhimu, kwani Hijjah yenye kukubaliwa haina jazaa ila
pepo.
b) Tahadharini na adui yenu mkuu
shetani asije kutusha baina yenu mjadala na mabishano yatakayosababisha uadui
na chuki baina yenu: “HIJJAH NI MIEZI MAALUMU, NA ANAYEKUSUDIA KUFANYA HIJJAH
KATIKA (miezi) HIYO, BASI ASISEME MANENO MACHAFU WALA ASIFANYE VITENDO
VICHAFU WALA ASIBISHANE KATIKA HIYO HIJJAH...” [2:197]
c) Waulizeni
wanazuoni wenu mlioambatana nao mas-ala tata yanayokutatizeni katika
utekelezaji mzima wa ibada yenu ili muweze kuitekeleza kama itakiwavyo na
sheria: “...BASI WAULIZENI WENYE KUMBUKUMBU (wenye kujua) IKIWA NYINYI HAMJUI”.
[16:43]
d) Eleweni kwamba Allah
ametufaradhishia baadhi ya mambo na kutusunishia mengine. Ni dhahiri shahiri
kwamba Allah hazikubali sunah za mtu aliyezivunja na kuzipoteza fardhi. Baadhi
ya mahujaji hughafilika na ukweli huu, wakawakera na kuwaudhi waumini wenziwao
na pengine kuhatarisha maisha yao kwa ajili tu ya kutaka kulibusu
“Hajarul-Aswad”. Au kwa ajili tu ya kutaka kwenda jarambe katika Twawaafu au
kuswali nyuma ya “Maqaamu Ibrahiym” au kunywa maji ya Zamzam. Fahamuni kwamba
mambo yote haya ni SUNAH na kuwaudhi waumini ni HARAMU, vipi basi tunatenda la
haramu kwa ajili ya kupata la Sunah?!
e) Tambueni
kwamba haitakikani mwanamume kuswali pembeni ya mwanamke au nyuma yake ndani ya
msikiti mtukufu au mahala pengine kwa sababu yo yote ile iwayo, ikiwa kuna
imkani ya kuliepuka hilo basi liepuke kadiri uwezavyo. Na enyi mahujaji
wanawake pupieni sana kuswali nyuma ya wanamume kama mtakiwavyo na sheria
tukufu.
f) Ni kheri kwenu nyinyi ikiwa mtakumbuka kwamba milango na maingilio ya
Haram (eneo takatifu) ni njia ambazo si halali kwa ye yote miongoni mwenu
kuziziba. Asiizibe milango/maingilio hayo kwa kuswali hapo hata kama ikiwa ni
kwa ajili ya kuidiriki swala ya jamaa.
g) Haijuzu
kuzuia/kuchelewesha utekelezaji wa ibada ya Twawaafu kwa kukaa pembezoni mwa
Al-Ka’abah au kwa kuswali karibu yake au kwa kusimama katika “Hijri-Ismail” au
“Maqaamu Ibraahiym”. Kuwa kwako au kuswali maeneo hayo husababisha kero na
usumbufu mkubwa usio wa lazima kwa wenzako wanaotufu khasa wakati wa
msongamano.
Haya ni baadhi tu ya mambo ambayo
Website yako {WEBSITE UISLAMU} imeonelea ni vema ikakukumbusha ili uweze kuitekeleza
ibada yako ya Hijjah kwa ufanisi mkubwa.
2. NAMNA YA KUITEKELEZA IBADA YA HIJJAH NA UMRAH:
Ewe Haji-Allah akutakabalie Hijjah
yako-kabla hatujaanza kukuelekeza utekelezaji wa ibada mbili hizi; Hijjah na
Umrah, ni vema tukajifunza kwanza pamoja:
a) Aina za
utekelezaji wa Hijjah na Umrah:
Kuna aina tatu za namna ya utekelezaji wa ibada za Hijjah na Umrah kama
zilivyofundishwa na Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-kwani yeye ndiye
aliyesema: “Twaeni kwangu ibada zenu” – yaani nitakavyofanya mimi nanyi
mfuate hivyo.
TAMATUI: Hii ndio aina ya kwanza, nako ni kuhirimia Umrah kwenye Miiqaati
(Ihram site) katika miezi ya Hijjah ambayo ni Shawwaal (Mfunguo mosi),
Dhul-Qa’adah (Mfunguo pili) na Dhul-Hijjah (Mfunguo tatu). Baada ya kutekeleza
ibada hii ya Umrah na kupata “Tahalul” (Release from Ihram) ndipo tena mtu
atahirimia Hijjah Makkah au karibu ya Makkah siku ya Tar-wiyah (mwezi 8 Mfunguo
tatu) katika mwaka ule ule aliofanya Umrah. Kwa kuitekeleza kwake ibada ya
Umrah na Hijjah kwa njia hii ya TAMATUI, kutamlazimu kuchinja mnyama “Hadiyu” –
(a voluntary sacrifice animal). Atamchinja mnyama huyu Minaa au sehemu nyingine
yo yote ya Haram siku ya kuchinja (mwezi 10 Mfunguo tatu) au baada yake katika siku
za “Tashriyq”. Siku za Tashriyq, hizi ni siku za kuanika nyama nazo ni zile
siku tatu zinazoiandamia Eidil-Hajji, yaani mwezi 11, 12 na 13. Kama hana
mnyama wa kuchinja basi na afunge siku kumi; tatu kule kule Makkah na saba
atakaporudi nyumbani, amesema Allah Mola Mtukufu: “...BASI MWENYE
KUJISTAREHESHA (tamatui) KWA KUFANYA UMRAH KISHA NDIO AKAHIJI, BASI ACHINJE
MNYAMA ALIYE SAHILIKA (nae ni mbuzi) NA ASIYEPATA, AFUNGE SIKU TATU KATIKA
HIJJAH NA SIKU SABA MTAKAPORUDI (kwenu); HIZI NI KUMI KAMILI”. [2:196]
QIRAANI: Hii ndio aina ya pili, huku ni kuhirimia Hijjah na Umrah pamoja.
Mwenye kuzitekeleza ibada mbili hizi; Hijjah na Umrah hapati Tahalul yaani
ahalalikiwi na yale yote yanayokuwa haramu kwake kuyatenda baada tu ya
kuhirimia ila siku ile ya kuchinja. Atapata Tahalul siku hiyo ya mwezi 10
Mfunguo tatu baada ya kutupia mawe “Jamratul-Aqabah” na kunyoa au kupunguza.
Huyu nae kutamlazimu kuchinja mnyama (Hadyu) Minaa au sehemu nyingine yo yote
ya Haram.
IFRAAD: Hii ndio aina ya tatu, huku ni kuhirimia Hijjah peke yake katika
Miiqaat (vituo vya kuhirimia), kisha Hajji ataendelea kubakia na Ihramu yake
mpaka siku ya kuchinja. Halafu ndio atafanya ibada ya Umrah.
Mukhtasari
wa kauli:
Þ Ifraadi ni mtu
kuhiji kwanza kisha ndio afanye Umrah.
Þ Tamatui ni mtu
kufanya Umrah kwanza kisha ndio ahiji.
Þ Qiraani ni mtu
kuhirimia Hijjah na Umrah; zote mbili kwa pamoja.
A. NAMNA YA KUFANYA UMRAH:
F Utakapofika kwenye Miiqaati (vituo vya kuhirimia) koga
na ujitie manukato likikuwepesikia hilo. Kisha vaa nguo za Ihraam ambazo ni
shuka mbili; moja ya kujifunga kiunoni na nyingine ni ya kujitanda na ni bora
sana ikiwa zote zitakuwa nyeupe. Ama mwanamke yeye atavaa nguo zo zote za
sitara azitakazo zisizo dhihirisha pambo lake. Kisha ndipo unuie kuhirimia
Umrah moyoni mwako kwa kusema:
“NAWAYTUL-UMRATA WA AHRAMTU BIHAA
LILLAAHI TAALA”.
Kisha utasema:
“LABBAYKA UMRATAN [LABBAYKAL-LAAHUMMA LABBAYKA,
LABBAYKA LAA SHARIYKA LAKA LABBAYKA, INNAL-HAMDA WAN-NI’IMATA LAKA WAL-MULKU,
LAA SHARIYKA LAKA”.
Wanaume wataijihirisha (wataileta
kwa sauti) Talbiyah hii na wanawake wataisirisha. Kisha kithirisha kuleta
Talbiyah, Dhikri, Istighfaari, kuamrisha mema na kukataza maovu.
F Kisha utaondoka hapo katika kituo chako cha kuhirimia
na kuelekea Makkah. Ukifika Makkah itufu Al-Ka’abah mara saba (Twawaafu ya
Umrah). Utaanzia kutufu kwenye “Hajarul-Aswad”, huku ukileta Takbira; yaani
ukisema Allaahu Akbar na kumalizia hapo, hiyo ni mara moja. Utafanya hivi hivi
kwa mara nyingine zilizobakia mpaka
zitimie saba. Wakati wa kutufu utamdhukuru Allah na kumuomba kwa dhikri na dua
yo yote uiwezayo. Lakini ni bora ukaikhitimisha kila mara (mzunguko mmoja) kwa
kusema:
“RABBANAA AATINAA FID-DUNYAA HASANATAN WAFIL-AAKHIRATI
HASANATAN WAQINAA ADHAABAN-NAARI”.
Katika utekelezaji wa zoezi zima
la Twawaafu hakikisha unachunga mambo yafuatayo:
a) Kulibusu
“Hajarul-Aswad” kama inamkinika, kama haimkiniki kunatosha kuligusa kwa mkono
tu. Hili pia kama likishindikana, kunakutosha kuliashiria kwa mkono pamoja na
kukabiri (kuleta Takbira). Kumbuka hakujuzu kuwazonga na kuwaudhi watu kwa
ajili ya kulibusu au kuligusa “Hajarul-Aswad”.
b) Kutufu kwa nyuma ya
“Hijril-Ismaail” na wala si ndani yake kwani hiyo ni sehemu ya Al-Ka’abah.
Ukimaliza kutufu swali rakaa mbili za Twawaafu nyuma ya “Maqaamu Ibraahiym”,
likiwepesika hilo kama haikuwezekana basi swali mahala po pote msikitini.
F Ukimaliza kuswali, ondoka ukiendee kilima Swafaa,
panda juu yake (zoezi hili ni kwa mwanamume pekee na wala halimkhusu mwanamke).
Elekea Qiblah, muhimidi Allah na umkabiri mara tatu ilhali umeinua mikono yako
ukiomba dua, kisha sema:
“LAA ILAAHA ILLAL-LAAHU WAHDAHU LAA SHARIYKA LAHUU,
LAHUL-MULKU WALAHUL-HAMDU WAHUWA ‘ALAA KULLI SHAIN QADIYRU. LAA ILAAHA
ILLAL-LAAHU WAHDAHU ANJAZA WA’ADAHU WANASWARA ‘ABDAHU WAHAZAMAL-AHZAABA
WAHDAH”.
Yakariri maneno haya mara tatu,
kisha shuka kilimani ili uanze kufanya Sa’ayi ya Umrah mara saba. Anzia hapo
Swafaa na kuishia Mar-wa, hiyo ni mara moja. Halafu toka hapo Mar-wa kurudi
Swafaa, hii ni mara ya pili. Endelea kufanya hivi kwa mara nyingine zilizobakia
mpaka zitimie saba. Nenda mwendo wa kawaida mpaka ukifika kwenye alama ya
kijani utakwenda matiti (jaramba/mbio) mpaka uifikie alama ya pili ya taa ya
kijani, hapo utatembea mwendo wa kawaida. Kumbuka zoezi hili linamkhusu
mwanaume tu (yaani huku kwenda matiti) na sio mwanamke. Angalia ukifika Mar-wa
utapanda juu yake kiasi na utayafanya yote uliyoyafanya Swafaa.
TANBIHI: Twawaafu na Sa’ayi hazina adhkari
(nyiradi) makhsusi za wajibu, bali mtu ataleta dhikri na dua zinazomuwepesikia
au atasoma Qur-ani.
F Ukishaikamilisha Sa’ayi yako, nyoa au punguza nywele.
Mpaka hapa Umrah yako itakuwa imekamilika, hivi ni iwapo umeifanya ibada yako
kwa njia ya Tamatui. Kwa kitendo chako cha kunyoa au kupunguza utakuwa umepata
“Tahalul”, yaani utakuwa umepata uhalali wa kuyafanya yale yote yaliyokuwa
haramu kuyafanya kwa sababu ya Ihraamu (things unlawful while in Ihraam). Ama
mtu aliyechagua kufanya ibada mbili hizi kwa njia ya Ifraadi au Qiraani, yeye
ataendelea kubakia na Ihraamu ya ibada ya Hijjah, wala hatapata Tahalul mpaka
siku ya kuchinja (mwezi 10 Mfunguo tatu). Huu ndio utaratibu wa kuitekeleza
ibada ya Umrah, sasa tuangalie yafuatayo:
Nguzo
za Umrah.
Nguzo za Umrah ni kama zifuatazo:
1. Ihraamu: Hii ni
NIA ya kuingia katika ibada husika kwa kutamka moyoni: – NAWAYTUL-UMRATA
WA AHRAMTU BIHAA LILLAAHI TAALA.
2. Twawaafu: Hili
ni zoezi la kuizunguka Al-Ka’abah tukufu mara saba kwa namna ilivyoelezwa
katika vitabu vya sheria.
3. Sa’ayi: Hili
ni zoezi la kwenda na kurudi mara saba baina ya vilima Swafaa na Mar-wa kwa
kufuata utaratibu uliowekwa na sheria.
4. Kunyoa au kupunguza: Hili ni zoezi linalohusisha uondoshaji wa nywele zote kichwani au
baadhi yake tu. Bora kwa mwanamume ni kunyoa na kwa mwanamke ni kupunguza
kidogo tu.
B. NAMNA YA KUHIJI:
F Ikiwa wewe umechagua kuifanya ibada ya Hijjah kwa njia
ya Ifraadi au Qiraani, basi hirimia Hijjah katika Miiqaati (Ihraamu sites)
unayoingilia Makkah. Iwapo hauko katika Miiqaati, basi hirimia ulichokinuia
mahala ulipo ndani ya mipaka ya Haram. Na ikiwa umechagua njia ya Tamatui, basi
utahirimia Hijjah mahala ulipo siku ya Tarwiyah ambayo ni mwezi 8 Mfunguo tatu.
F Baada ya kuhirimia, koga na ujitie manukato
likikuwepesikia hilo. Kisha vaa vazi la Ihraamu, halafu sema:
“LABBAYKA HAJJAN,
LABBAYKAL-LAAHUMMA LABBAYKA, LABBAYKA LAA SHARIYKA LAKA LABBAYKA, INNAL-HAMDA
WAN-NI’IMATA LAKA WAL-MULKU LAA SHARIYKA LAKA”.
F Halafu ondoka uelekee Minaa na uswali hapo swala za
Adhuhuri, Alasiri, Maghribi, Ishaa na Alfajiri ya mwezi tisaa. Utazikusuru
swala za rakaa nne kwa kuziswali rakaa mbili mbili katika nyakati zake bila ya
kuzijumuisha.
F Litakapochomoza jua mwezi tisaa Mfunguo tatu, ondoka
Minaa na uelekee katika viwanja vya Arafah kwa utulivu bila ya kuwaudhi
mahujaji wenzio. Utaswali hapo swala za Adhuhuri na Laasiri kwa kuzijumuisha
mjumuisho wa kutanguliza na kuzikusuru (yaani kuziswali rakaa mbili mbili
badala ya nne nne). Ni wajibu uhakikishe kuwa umeingia na umo ndani ya mipaka
ya Arafah, uwe makini sana khususan upande wa Kaskazini na Mashariki. Arafah
yote ni mahala pa kusimama isipokuwa mahala panapoitwa “Batwni Arinah”. Ni
kheri kwako ikiwa utafahamu kwamba kusimama Arafah ndio nguzo kuu ya Hijjah
kutokana na kauli yake Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie: “Hijjah ni
Arafah”. Kutokana na kauli hii ya Mtume wa Allah itakuwazikia kwamba mtu
ambaye hakusimama katika viwanja vya Arafah mchana baada ya swala ya Adhuhuri
au usiku mpaka kuchomoza kwa Alfajiri ya siku ya kuchinja (mwezi 10), hana
Hijjah mtu huyo. Cha kufanya hapo Arafah ni kukithirisha mno kuleta adhkaari na
dua, ilhali umeelekea Qiblah ukiwa umenyanyua mikono yako kama alivyofanya
Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie. Endelea kubakia hapo Arafah mpaka kuchwa
kwa jua.
F Jua likishazama, shika njia kuelekea Muzdalifah kwa
upole na utuvu mkubwa huku ukileta Talbiyah na tahadhari usiwaudhi mahujaji
wenzako: “...NA MTAKAPORUDI KUTOKA ARAFAATI MTAJENI (mdhukuruni) ALLAH PENYE
MASH’ARIL HARAAM...” [2:198] Utaswali hapa Muzdalifah swala za Maghribi na
Ishaa kwa kuzijumuisha mjumuisho wa kuakhirisha, yaani uziswali swala mbili
hizo zote; Maghribi na Ishaa katika wakati wa Ishaa. Utaziswali kwa adhana moja
na Iqaamah mbili; Iqaamah moja kwa ajili ya Maghribi na nyingine kwa ajili ya
Ishaa. Utabakia hapa mpaka kuswali Alfajiri ukikithirisha dhikri na dua.
F Kisha ondoka kabla ya kuchomoza kwa jua la siku hii ya
mwezi 10 Mfunguo 3; siku ya Eidil-Adh-haa uelekee Minaa huku ukileta Talbiyah.
Ukiwa una udhuru, mathalan umeambatana na wanawake au madhaifu (wakongwe,
walemavu n.k.) si vibaya ikiwa utaanza kuelekea Minaa tangu baada ya saa sita
usiku. Chukua hapa Muzdalifah vijiwe saba (pebbles) kwa ajili ya kwenda
kutupia “Jamratul-Aqabah”, vijiwe
vingine utachukua huko huko Minaa.
F Ukishafika Minaa unatakiwa kufanya mambo yafuatayo:
1. Kitupie/kipige
mawe kinara cha Jamratul-Aqabah, hiki ni kile kilicho karibu na Makkah.
Utakipiga mawe saba, yenye kufuatana moja baada ya jingine huku ukileta Takbiri
na sio kuyatupa yote kwa mkupuo mmoja tu.
2. Chinja
mnyama (hadyu) ikiwa umelazimikiwa kutokana na kuifanya ibada ya Hijjah na
Umrah kwa njia ya Tamatui au Qiraani. Ule sehemu ya nyama hiyo wewe mwenyewe na
iliyobakia walishe mafakiri.
3. Nyoa au
punguza nywele, lakini kunyoa ni bora zaidi kwa mwanamume na mwanamke yeye
atapunguza nywele kiasi kidogo tu.
Baada ya kutupia mawe
Jamratul-Aqabah na kunyoa au kupunguza utakuwa umepata Tahalul ya kwanza, yaani
utakuwa umepata uhalali wa kuyafanya yale yote uliyokuwa umezuiwa kwa sababu ya
Ihraamu ila kumuingilia mkeo.
4. Kisha
teremka Makkah na utufu “Twawaaful-Ifaadhwah” mara saba, hii ni Twawaafu ya
nguzo, kwani Hijjah yako haitimii ila kwa kuileta/kuitenda. Halafu ufanye
Sa’ayi baina ya Swafaa na Mar-wa mara saba, hii ni iwapo ulichagua kufanya
ibada mbili hizi; Hijjah na Umrah kwa njia ya Tamatui. Kadhalika kutampasa
kufanya Sa’ayi yule aliyeichagua njia ya Qiraani au Ifraadi, iwapo hakufanya
Sa’ayi baada ya Twawaful-Quduum. Baada ya Sa’ayi hii, ndipo utapata Tahalul ya
pili ambayo itakuhalalishia mambo yote hata kumuingilia mkeo.
5. Baada
ya kutufu Al-Ka’abah Twaaful-Ifaadhwah siku ya kuchinja, rejea Minaa na ulale
hapo usiku wa mwezi 11, 12 na 13 (masiku ya kuanika nyama – Ayyaamut-tashriyq).
Kunajuzu pia kulala nyusiku mbili tu, yaani usiku wa mwezi 11 na 12. Hapa
utavitupia mawe vinara vyote vitatu kila siku baada ya kupinduka jua, kila
kinara utakitupia mawe saba; moja baada ya jingine huku ukileta Takbira kwa
kila jiwe unalotupa. Utaanza kukitupia mawe kinara cha kwanza, siku ya mwezi
11, hiki ni kile kinachouandamia msikiti wa Hunayfi. Kisha utakitupia kinara
cha kati na utamalizia na Jamratul-Aqabah. Utafanya hivi katika siku
inayofuatia, yaani mwezi 12. Ikiwa una haraka, utaondoka kuelekea Makkah baada
ya kuvitupia mawe vinara siku hiyo ya mwezi 12. Kuondoka huku ni sharti kuwe
kabla ya kuzama kwa jua, ikiwa utachelewa mpaka jua likazama ukawa bado
haujaondoka Minaa, basi kutakulazimu kulala hapo hapo Minaa na uvitupie mawe
vinara baada ya kupinduka kwa jua siku ya mwezi 13. Hapo sasa ndio unaweza
kuondoka Minaa kurudi Makkah: “NA MTAJENI ALLAH KATIKA ZILE SIKU
ZINAZOHISABIWA, LAKINI AFANYAYE HARAKA KATIKA SIKU MBILI (akarejea) BASI SI
DHAMBI JUU YAKE, NA MWENYE KUKAWIA PIA SI DHAMBI JUU YAKE, KWA MWENYE KUMCHA
ALLAH...” [2:203] Baada ya kumaliza amali zote hizi za ibada ya Hijjah na Umrah
na ukaazimia kufunga safari ya kurudi nyumbani, kunakuwajibikia kutufu
“Twawaaful-Wadaai” ambayo hasameheki kuiacha ila mwanamke mwenye damu ya hedhi
au nifasi tu. Mpaka hapa utakuwa umeikamilisha Hijjah yako.
Nguzo za Hijjah.
Ibada ya Hijjah imesimama juu ya
nguzo zifuatazo:
1. Kuhirimia.
2. Kutufu “Twawaaful-Ifaadhwah”,
3. Kusa’ayi baina ya Swafaa na Mar-wa.
4. Kusimama Arafah.
5. Kunyoa au kupunguza.
Waajibaati za Hijjah.
1. Kuhirimia katika Miiqaati.
2. Kulala Muzdalifah usiku wa Idi.
3. Kulala Minaa katika masiku ya Tashriyq.
4. Kutupia mawe vinara.
5. Kutufu “Twawaaful-Wadaai”.
6. Kujiepusha na Muharamaati za Ihraamu (mambo yaliyo haramishwa kwa sababu
ya Ihraamu).
7. Kunyoa au kupunguza.
Elewa na uzingatie kwamba Haji
akiacha mojawapo ya nguzo za Hijjah, Hijjah yake hiyo haitasihi kisheria ila
kwa kuitenda hiyo nguzo aliyoiacha. Na akiacha mojawapo ya Waajibaati zake,
Hijjah yake itasihi lakini kutamlazimu kuchinja mnyama Makkah.
Yanayomuwajibikia
mwenye kuhirimia.
Yanamuwajibikia mtu mwenye kuhirimia ibada ya Hijjah
na Umrah mambo yafuatayo:
1. Ajilazimishe kuyatenda yale yote aliyowajibishiwa na Mola wake katika
fardhi za dini yake kama vile kuswali swala kwa nyakati zake tena katika jamaa.
2. Ajiepushe na yale yote aliyokatazwa na Allah, asiseme maneno machafu,
asifanye vitendo vichafu (ufasiki), asifanya mjadala muovu utakaopelekea uadui,
na..... na......
3. Ajiepushe na Muharaamati za Ihraamu (things unlawful while in Ihraam).
Mambo yanayomuharamikia mwenye kuhirimia kwa sababu ya huko kuhirimia kwake
Hijjah ni kama yafuatayo:
a) Kunyoa/kukata nywele au kucha hata kidogo tu.
b) Kujitia manukato mwilini au nguoni. Haidhuru athari ya manukato
aliyojitia kabla ya kuhirimia.
c) Kuwinda na kumuua mnyama au ndege wa bara au kumsaidia mtu kufanya
hivyo.
d) Kukata au kung’oa mimea ya Haram.
e) Kuposa au kufunga ndoa yeye mwenyewe au kwa ajili ya mtu mwingine.
f) Kumuingilia mkewe.
Haya yanawakhusu wote; mwanamume
na mwanamke. Haya yafuatayo yanamkhusu mwanamume tu:
a) Kufunika
kichwa chake kwa kuvaa kitu mithili ya kofia au kilemba. Ama kutumia mwavuli si
vibaya.
b) Kuvaa nguo zilizoshonwa (sewn
garments).
Ama mwanamke, yeye anakhusika na
yafuatayo:
a) Kuvaa
gloves mikononi.
b) Kufunika uso.
Kunajuzu kwa mwenye kuhirimia
kuvaa kandambili/viatu, pete, miwani, saa na mkanda wa kuhifadhia pesa.
Subscribe to:
Posts (Atom)