Thursday, October 17, 2013

SHEIKH JONGO ABEBESHA WAISLAMU ZIGO



Kadhi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Hamid Jongo, amepinga madai, ambayo yamekuwa yakitolewa na baadhi ya watu kwamba, ndani ya serikali kuna mtandao wa Wakristo, ambao wanawachukia Waislamu na kusema wenye matatizo ni Waislamu wenyewe.

Sheikh Jongo, ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza la Ulamaa la Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), alisema hayo wakati akihutubia katika sherehe za Baraza la Idi el-Hajj, zilizofanyika katika Msikiti wa Al-Farouq, Makao Makuu ya Bakwata, Kinondoni, jijini Dar es Salaam jana.

Alisema kwa mujibu wa utafiti alioufanya hakuna mtandao wa Wakristo ndani ya serikali, ila mtandao unaweza kuwapo ndani ya Wakristo wenyewe kama ambavyo unaweza pia kuwapo ndani ya Waislamu na si serikalini.

Sheikh Jongo alisema kinyume cha madai hayo, ukweli uliopo ni kwamba, Waislamu wenyewe ndiyo wenye matatizo, ambao hawana nidhamu, utaratibu na uongozi kiasi ambacho kila mmoja amekuwa mwamuzi wa mambo yanayohusu Uislamu.

Alisema inashangaza kuona leo Mufti anatangaza kuwa kesho ndiyo Idi, baadhi ya Waislamu wanasema leo.

 “Wakristo, serikali, CCM hawana matatizo hata kidogo. Wenye matatizo ni sisi wenyewe  Waislamu,” alisema Sheikh Jongo.

Alisema matajiri wengi nchini ni Waislamu, lakini Waislamu wanashindwa kuwaendea kuwaomba wawasaidie mambo ya kimaendeleo, kama vile elimu, badala yake wanawaendea kwa ajili ya kuomba misaada ili wakaoe, jambo ambalo alisema matajiri ‘wamelishtukia’.

 “Tusiwadhulumu Wakristo. Kama wanaimarisha dini yao na sisi tuimarishe dini yetu. Chuo Kikuu Morogoro katupa Mkapa Mkristo. Lakini sisi wenyewe hata chumba kimoja hatuna,” alisema Sheikh Jongo.

Alisema Waislamu wanamiliki maghala mengi, ambayo wanaweza kuyatumia kuanzisha vyuo vikuu na kuhoji: “Kwanini hatuanzishi Chuo Kikuu?”

 Sheikh Jongo alisema iwapo Waislamu wenyewe watatumia rasilimali walizonazo kuanzisha Chuo Kikuu kisha serikali ikawanyima, wataandamana na yeye ndiye atakayeongoza hayo maandamano.

Alisema maadui wa Waislamu waliotajwa na Kur’ani Tukufu ni shetani na Mayahudi na kuhoji: “Umepata wapi Wakristo ni maadui wa Waislamu?”

“Uislamu huu unaofanywa na wapigadebe siyo ule aliokuja nao Mtume S.A.W. Uislamu wa Mtume ni amani na utulivu,” alisema Sheikh Jongo.

Awali, akiwasilisha salamu za Bakwata katika sherehe hizo, Katibu Mkuu wa Bakwata, Ustadh Suleiman Lolila, aliiomba serikali kusitisha utekelezaji wa kanuni mpya za mtihani za mwaka 2013, ambazo zimeyapanga baadhi ya masomo, yakiwamo ya dini zote katika kundi la hiari.

Alisema kwa mujibu wa kanuni hizo mpya za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, masomo ya dini zote, lugha ya Kiarabu, Kifaransa na Kompyuta, hayatatumika katika kutunuku ufaulu wa wanafunzi, hasa katika kumpangia daraja.

“Tunaomba Wizara ya Elimu isitishe utekelezaji wa zoezi hili kama ilivyoainishwa katika Examination Regulations (kanuni za mtihani) ya mwaka 2013 hadi hapo mazungumzo kati ya wakuu wa taasisi za dini zote zenye shule na Wizara ya Elimu yatakapofanyika kwa manufaa ya taifa letu.

Tunaiomba Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi iharakishe kuitisha  kikao hicho na kufikia mwafaka kwa mustakabali mwema wa taifa letu,” alisema Ustadh Lolila.

Alisema dini ndiyo inayowajenga watoto na raia wa kesho kimaadili, hivyo wangetegemea serikali kuweka mkazo katika masomo hayo ili yatahiniwe na kumpa mwanafunzi ufaulu wa kusonga mbele na hapo hapo kumsaidia kujenga maadili mema ya Taifa kwa vijana.

Alisema pia wanafunzi wa shule za msingi kwa kujua kwamba, masomo hayo hayana tija, wakifika sekondari, ni rahisi kupuuzia kusoma masomo ya dini na kwamba, tatizo la maadili litaongezeka katika jamii endapo masomo ya dini hayatatahiniwa.

Alisema pia vyuo vikuu vya ualimu nchini, kama vile Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro, Chuo Kikuu cha Zanzibar na vyuo kadhaa vya ualimu vyenye mitaala hiyo vitakosa wanafunzi.

Alisema vilevile, vyuo vingi vitaathirika na idadi ya Watanzania wanaokwenda vyuo vikuu kupungua sana.

Alisema wapo pia Watanzania wanaojiunga na vyuo vya kimataifa vinavyotumia mchepuo wa masomo ya dini kama Chuo Kikuu cha Makerere, vyuo vikuu vya Sudan na Misri na kwingine ulimwenguni kote, wataathirika vibaya na uamuzi huo wa serikali.

 Akijibu hilo, Waziri wa Maji, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika sherehe hizo, Profesa Jumanne Maghembe, alisema amelipokea na kwamba, atalifikisha kwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, haraka iwezekanvyo na kwamba, suala waliloomba litapatiwa ufumbuzi.

Hata hivyo, alisema mchango wa Waislamu katika elimu haulingani na uwezo na wingi walionao, hivyo akawaomba waisaidie serikali kuandaa wataalamu na vijana kutoa mafundisho ya dini ya Kiislamu.

Naye Kaimu Mufti wa Tanzania, Sheikh Ismail Habib Makusanya, alisema tofauti na huko nyuma, hivi sasa kuna dalili za kuvunjika amani na utulivu kunakofanywa na baadhi ya watu nchini, hivyo akaishauri serikali kuwa wakali ili kuwadhibiti watu wa aina hiyo.
Chanzo:Nipashe

No comments: