Tuesday, September 17, 2013

MAKALA MAALUM-IBADA TUKUFU YA HIJJA



Ibada ya Hijjah ndio inayozikamilisha nguzo tano za Uislamu, amesema Allah Mola Mwenyezi: “...NA ALLAH AMEWAWAJIBISHIA WATU WAFANYE HIJJAH KATIKA NYUMBA HIYO; YULE AWEZAYE KUFUNGA SAFARI KWENDA HUKO...” [3:97] Na akasema tena: “NA (tukamwambia): UTANGAZE KWA WATU KHABARI ZA HIJJAH, WATAKUJIA (wengine) KWA MIGUU NA (wengine) JUU YA KILA MNYAMA ALIYECHOKA (kwa machofu ya njiani) WAKIJA KUTOKA KATIKA KILA NJIA YA MBALI. ILI WASHUHUDIE MANUFAA YAO NA (ili wakithirishe) KULITAJA JINA LA ALLAH KATIKA SIKU ZINAZOJULIKANA...” [22:27-28] Imepokewa kutoka kwa Abu Hurayrah-Allah amuwiye radhi-amesema-Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Enyi watu! Hakika Allah amekufaradhishieni Hijjah, basi hijini (nendeni Hijjah). Atakayehiji kwa ajili tu (ya kutaka radhi za) Allah na asiseme maneno machafu wala asifanye vitendo vichafu, atatoka katika madhambi yake kama siku aliyozaliwa na mama yake. Na Umrah moja mpaka nyingine ni kafara ya madhambi ya kipindi kilicho baina ya (Umrah) mbili hizo na Hijjah yenye kukubaliwa haina jazaa (malipo) ila pepo”. Bukhaariy & Muslim-Allah awarehemu.
Katika mithili ya masiku kama haya kila mwaka, macho, masikio na nyoyo za waislamu ulimwenguni kote huelekezwa nchini Saudi Arabia. Khususan katika mji Mtakatifu wa Makkah; mahala ambapo ipo nyumba takatifu na kongwe ya Allah, nyumba inayotajwa na kauli tukufu ya Allah: “KWA YAKINI NYUMBA YA KWANZA ILIYOWEKWA KWA AJILI YA WATU (kufanya ibada) NI ILE ILIYOKO MAKKAH, YENYE BARAKA NA UONGOZI KWA AJILI YA WALIMWENGU WOTE. HUMO MNA ISHARA ZILIZO WAZI (za kuonyesha utukufu wake na ukongwe wake. Miongoni mwa hizo ni) MAHALA ALIPOKUWA AKISIMAMA IBRAHIMU, NA ANAYEINGIA (Haram) ANAKUWA KATIKA SALAMA...” [3:96-97]
Waja wa Allah huuitikia wito wa Mola wao katika masiku haya kwa kufunga safari kutoka pande mbalimbali za dunia kuielekea nyumba hii tukufu ya Allah. Huenda huko kwa ajili tu ya kuitekeleza ibada ya Hijah ambayo ni nguzo ya tano ya Uislamu; dini na mfumo wao sahihi wa maisha. Ibada hii tukufu huwakutanisha pamoja ndugu wa imani wa mataifa, lugha, hadhi na rangi mbalimbali. Huu ni mkutano na mkusanyiko usio na mithali yake katika ulimwengu huu, ulimwenguni kote haujapata na wala hautapata kutokea mkusanyiko unaowakusanya watu wengi na wa mataifa mengi kama huu wa Hijjah. Kutokana na utukufu na umuhimu wa ibada hii tukufu ya Hijjah, Website yako (WEBSITE UISLAMU) inajifakharisha kwa mara nyingine tena kuifanyia kazi kauli tukufu ya Allah: “...NA SAIDIANENI KATIKA WEMA NA TAQWA, WALA MSISAIDIANE KATIKA MADHAMBI NA UADUI”. [5:2] Ili kukusaidia wewe ndugu mpenzi Hajji kuitekeleza kauli ya Allah Mola Mlezi wako: “NA TIMIZENI HIJJAH NA UMRAH KWA AJILI YA ALLAH...” [2:196] Website yako inakuletea maelezo haya mukhtasari inayopenda kuyaita (MUONGOZO WA HIJJAH NA UMRAH) huku ikiamini kwa yakini kwamba inachangia katika suala zima la kusaidiana katika WEMA na TAQWA. Ni matumaini ya Website Uislamu kwamba utaupokea muongozo huu kwa mikono miwili na kupupia kuusoma kwa nia ya kujifunza, kujua na kuutumia katika kipindi chote cha kuitekeleza kwako ibada hii tukufu. Kadhalika ni matarajio ya Website Uislamu kuwa muongozo huu utakupa msaada mkubwa utakaokuwezesha kuitekeleza ibada hii  kwa UJUZI WA KWELI. Website Uislamu inawatakia mahujaji wote Hijjah njema iliyotakasika kwa ajili ya Allah. Haya sasa karibu katika MUONGOZO WA HIJJAH NA UMRAH, kwa jina la Allah na kwa kuutaraji mno msaada na taufiq yake tunaanza kwa:
 
  1. USIA MUHIMU:
         Enyi mahujaji, Website yenu (WEBSITE UISLAMU) inapenda kuitumia fursa hii adhimu kumuhimidi Allah aliyekuwafikisheni kwenda kuhiji katika nyumba yake tukufu. Kama alivyokuwafikisheni kuhiji tunamuomba akutakabalieni ibada yenu hii na baki ya amali nzenu njema, Aamiyn! Ili kuhakikisha kuwa unafuzu katika kuitekeleza ibada hii, tunapenda kwa mapenzi ya Allah kukupa wasia muhimu kama ifuatavyo:
a)      Kumbukeni kwamba nyinyi kama mahujaji mumo katika safari tukufu yenye baraka tele za Allah. Pia mumo katika Hijrah; mnaiacha miji yenu, watu wenu na shughuli zenu kwa ajili tu ya kuuitika wito wa Mola wenu. Fahamuni-Allah akurehemuni-kwamba safari yenu hii ina ujira adhimu, kwani Hijjah yenye kukubaliwa haina jazaa ila pepo.
b)     Tahadharini na adui yenu mkuu shetani asije kutusha baina yenu mjadala na mabishano yatakayosababisha uadui na chuki baina yenu: “HIJJAH NI MIEZI MAALUMU, NA ANAYEKUSUDIA KUFANYA HIJJAH KATIKA (miezi) HIYO, BASI ASISEME MANENO MACHAFU WALA ASIFANYE VITENDO VICHAFU WALA ASIBISHANE KATIKA HIYO HIJJAH...” [2:197]
c)      Waulizeni wanazuoni wenu mlioambatana nao mas-ala tata yanayokutatizeni katika utekelezaji mzima wa ibada yenu ili muweze kuitekeleza kama itakiwavyo na sheria: “...BASI WAULIZENI WENYE KUMBUKUMBU (wenye kujua) IKIWA NYINYI HAMJUI”. [16:43]
d)     Eleweni kwamba Allah ametufaradhishia baadhi ya mambo na kutusunishia mengine. Ni dhahiri shahiri kwamba Allah hazikubali sunah za mtu aliyezivunja na kuzipoteza fardhi. Baadhi ya mahujaji hughafilika na ukweli huu, wakawakera na kuwaudhi waumini wenziwao na pengine kuhatarisha maisha yao kwa ajili tu ya kutaka kulibusu “Hajarul-Aswad”. Au kwa ajili tu ya kutaka kwenda jarambe katika Twawaafu au kuswali nyuma ya “Maqaamu Ibrahiym” au kunywa maji ya Zamzam. Fahamuni kwamba mambo yote haya ni SUNAH na kuwaudhi waumini ni HARAMU, vipi basi tunatenda la haramu kwa ajili ya kupata la Sunah?!
e)      Tambueni kwamba haitakikani mwanamume kuswali pembeni ya mwanamke au nyuma yake ndani ya msikiti mtukufu au mahala pengine kwa sababu yo yote ile iwayo, ikiwa kuna imkani ya kuliepuka hilo basi liepuke kadiri uwezavyo. Na enyi mahujaji wanawake pupieni sana kuswali nyuma ya wanamume kama mtakiwavyo na sheria tukufu.
f)       Ni kheri kwenu nyinyi ikiwa mtakumbuka kwamba milango na maingilio ya Haram (eneo takatifu) ni njia ambazo si halali kwa ye yote miongoni mwenu kuziziba. Asiizibe milango/maingilio hayo kwa kuswali hapo hata kama ikiwa ni kwa ajili ya kuidiriki swala ya jamaa.
g)      Haijuzu kuzuia/kuchelewesha utekelezaji wa ibada ya Twawaafu kwa kukaa pembezoni mwa Al-Ka’abah au kwa kuswali karibu yake au kwa kusimama katika “Hijri-Ismail” au “Maqaamu Ibraahiym”. Kuwa kwako au kuswali maeneo hayo husababisha kero na usumbufu mkubwa usio wa lazima kwa wenzako wanaotufu khasa wakati wa msongamano.
Haya ni baadhi tu ya mambo ambayo Website yako {WEBSITE UISLAMU} imeonelea ni vema ikakukumbusha ili uweze kuitekeleza ibada yako ya Hijjah kwa ufanisi mkubwa.
 
2.         NAMNA YA KUITEKELEZA IBADA YA HIJJAH NA UMRAH:
             Ewe Haji-Allah akutakabalie Hijjah yako-kabla hatujaanza kukuelekeza utekelezaji wa ibada mbili hizi; Hijjah na Umrah, ni vema tukajifunza kwanza pamoja:
a)     Aina za utekelezaji wa Hijjah na Umrah:
         Kuna aina tatu za namna ya utekelezaji wa ibada za Hijjah na Umrah kama zilivyofundishwa na Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-kwani yeye ndiye aliyesema: “Twaeni kwangu ibada zenu” – yaani nitakavyofanya mimi nanyi mfuate hivyo.
TAMATUI: Hii ndio aina ya kwanza, nako ni kuhirimia Umrah kwenye Miiqaati (Ihram site) katika miezi ya Hijjah ambayo ni Shawwaal (Mfunguo mosi), Dhul-Qa’adah (Mfunguo pili) na Dhul-Hijjah (Mfunguo tatu). Baada ya kutekeleza ibada hii ya Umrah na kupata “Tahalul” (Release from Ihram) ndipo tena mtu atahirimia Hijjah Makkah au karibu ya Makkah siku ya Tar-wiyah (mwezi 8 Mfunguo tatu) katika mwaka ule ule aliofanya Umrah. Kwa kuitekeleza kwake ibada ya Umrah na Hijjah kwa njia hii ya TAMATUI, kutamlazimu kuchinja mnyama “Hadiyu” – (a voluntary sacrifice animal). Atamchinja mnyama huyu Minaa au sehemu nyingine yo yote ya Haram siku ya kuchinja (mwezi 10 Mfunguo tatu) au baada yake katika siku za “Tashriyq”. Siku za Tashriyq, hizi ni siku za kuanika nyama nazo ni zile siku tatu zinazoiandamia Eidil-Hajji, yaani mwezi 11, 12 na 13. Kama hana mnyama wa kuchinja basi na afunge siku kumi; tatu kule kule Makkah na saba atakaporudi nyumbani, amesema Allah Mola Mtukufu: “...BASI MWENYE KUJISTAREHESHA (tamatui) KWA KUFANYA UMRAH KISHA NDIO AKAHIJI, BASI ACHINJE MNYAMA ALIYE SAHILIKA (nae ni mbuzi) NA ASIYEPATA, AFUNGE SIKU TATU KATIKA HIJJAH NA SIKU SABA MTAKAPORUDI (kwenu); HIZI NI KUMI KAMILI”. [2:196]
QIRAANI: Hii ndio aina ya pili, huku ni kuhirimia Hijjah na Umrah pamoja. Mwenye kuzitekeleza ibada mbili hizi; Hijjah na Umrah hapati Tahalul yaani ahalalikiwi na yale yote yanayokuwa haramu kwake kuyatenda baada tu ya kuhirimia ila siku ile ya kuchinja. Atapata Tahalul siku hiyo ya mwezi 10 Mfunguo tatu baada ya kutupia mawe “Jamratul-Aqabah” na kunyoa au kupunguza. Huyu nae kutamlazimu kuchinja mnyama (Hadyu) Minaa au sehemu nyingine yo yote ya Haram.
 
IFRAAD: Hii ndio aina ya tatu, huku ni kuhirimia Hijjah peke yake katika Miiqaat (vituo vya kuhirimia), kisha Hajji ataendelea kubakia na Ihramu yake mpaka siku ya kuchinja. Halafu ndio atafanya ibada ya Umrah.

Mukhtasari wa kauli:
Þ    Ifraadi ni mtu kuhiji kwanza kisha ndio afanye Umrah.
Þ    Tamatui ni mtu kufanya Umrah kwanza kisha ndio ahiji.
Þ    Qiraani ni mtu kuhirimia Hijjah na Umrah; zote mbili kwa pamoja.
 
A.       NAMNA YA KUFANYA UMRAH:
F     Utakapofika kwenye Miiqaati (vituo vya kuhirimia) koga na ujitie manukato likikuwepesikia hilo. Kisha vaa nguo za Ihraam ambazo ni shuka mbili; moja ya kujifunga kiunoni na nyingine ni ya kujitanda na ni bora sana ikiwa zote zitakuwa nyeupe. Ama mwanamke yeye atavaa nguo zo zote za sitara azitakazo zisizo dhihirisha pambo lake. Kisha ndipo unuie kuhirimia Umrah moyoni mwako kwa kusema:                
“NAWAYTUL-UMRATA WA AHRAMTU BIHAA LILLAAHI TAALA”.
Kisha utasema: 
“LABBAYKA UMRATAN [LABBAYKAL-LAAHUMMA LABBAYKA, LABBAYKA LAA SHARIYKA LAKA LABBAYKA, INNAL-HAMDA WAN-NI’IMATA LAKA WAL-MULKU, LAA SHARIYKA LAKA”.
Wanaume wataijihirisha (wataileta kwa sauti) Talbiyah hii na wanawake wataisirisha. Kisha kithirisha kuleta Talbiyah, Dhikri, Istighfaari, kuamrisha mema na kukataza maovu.
 
F     Kisha utaondoka hapo katika kituo chako cha kuhirimia na kuelekea Makkah. Ukifika Makkah itufu Al-Ka’abah mara saba (Twawaafu ya Umrah). Utaanzia kutufu kwenye “Hajarul-Aswad”, huku ukileta Takbira; yaani ukisema Allaahu Akbar na kumalizia hapo, hiyo ni mara moja. Utafanya hivi hivi kwa  mara nyingine zilizobakia mpaka zitimie saba. Wakati wa kutufu utamdhukuru Allah na kumuomba kwa dhikri na dua yo yote uiwezayo. Lakini ni bora ukaikhitimisha kila mara (mzunguko mmoja) kwa kusema:                  
“RABBANAA AATINAA FID-DUNYAA HASANATAN WAFIL-AAKHIRATI HASANATAN WAQINAA ADHAABAN-NAARI”.
Katika utekelezaji wa zoezi zima la Twawaafu hakikisha unachunga mambo yafuatayo:
a)      Kulibusu “Hajarul-Aswad” kama inamkinika, kama haimkiniki kunatosha kuligusa kwa mkono tu. Hili pia kama likishindikana, kunakutosha kuliashiria kwa mkono pamoja na kukabiri (kuleta Takbira). Kumbuka hakujuzu kuwazonga na kuwaudhi watu kwa ajili ya kulibusu au kuligusa “Hajarul-Aswad”.
b)     Kutufu kwa nyuma ya “Hijril-Ismaail” na wala si ndani yake kwani hiyo ni sehemu ya Al-Ka’abah. Ukimaliza kutufu swali rakaa mbili za Twawaafu nyuma ya “Maqaamu Ibraahiym”, likiwepesika hilo kama haikuwezekana basi swali mahala po pote msikitini.
 
F     Ukimaliza kuswali, ondoka ukiendee kilima Swafaa, panda juu yake (zoezi hili ni kwa mwanamume pekee na wala halimkhusu mwanamke). Elekea Qiblah, muhimidi Allah na umkabiri mara tatu ilhali umeinua mikono yako ukiomba dua, kisha sema:
“LAA ILAAHA ILLAL-LAAHU WAHDAHU LAA SHARIYKA LAHUU, LAHUL-MULKU WALAHUL-HAMDU WAHUWA ‘ALAA KULLI SHAIN QADIYRU. LAA ILAAHA ILLAL-LAAHU WAHDAHU ANJAZA WA’ADAHU WANASWARA ‘ABDAHU WAHAZAMAL-AHZAABA WAHDAH”.
Yakariri maneno haya mara tatu, kisha shuka kilimani ili uanze kufanya Sa’ayi ya Umrah mara saba. Anzia hapo Swafaa na kuishia Mar-wa, hiyo ni mara moja. Halafu toka hapo Mar-wa kurudi Swafaa, hii ni mara ya pili. Endelea kufanya hivi kwa mara nyingine zilizobakia mpaka zitimie saba. Nenda mwendo wa kawaida mpaka ukifika kwenye alama ya kijani utakwenda matiti (jaramba/mbio) mpaka uifikie alama ya pili ya taa ya kijani, hapo utatembea mwendo wa kawaida. Kumbuka zoezi hili linamkhusu mwanaume tu (yaani huku kwenda matiti) na sio mwanamke. Angalia ukifika Mar-wa utapanda juu yake kiasi na utayafanya yote uliyoyafanya Swafaa.
TANBIHI: Twawaafu na Sa’ayi hazina adhkari (nyiradi) makhsusi za wajibu, bali mtu ataleta dhikri na dua zinazomuwepesikia au atasoma Qur-ani.
F     Ukishaikamilisha Sa’ayi yako, nyoa au punguza nywele. Mpaka hapa Umrah yako itakuwa imekamilika, hivi ni iwapo umeifanya ibada yako kwa njia ya Tamatui. Kwa kitendo chako cha kunyoa au kupunguza utakuwa umepata “Tahalul”, yaani utakuwa umepata uhalali wa kuyafanya yale yote yaliyokuwa haramu kuyafanya kwa sababu ya Ihraamu (things unlawful while in Ihraam). Ama mtu aliyechagua kufanya ibada mbili hizi kwa njia ya Ifraadi au Qiraani, yeye ataendelea kubakia na Ihraamu ya ibada ya Hijjah, wala hatapata Tahalul mpaka siku ya kuchinja (mwezi 10 Mfunguo tatu). Huu ndio utaratibu wa kuitekeleza ibada ya Umrah, sasa tuangalie yafuatayo:
 
Nguzo za Umrah.
 
Nguzo za Umrah ni kama zifuatazo:
1.         Ihraamu: Hii ni NIA ya kuingia katika ibada husika kwa kutamka moyoni: NAWAYTUL-UMRATA WA AHRAMTU BIHAA LILLAAHI TAALA.
2.         Twawaafu: Hili ni zoezi la kuizunguka Al-Ka’abah tukufu mara saba kwa namna ilivyoelezwa katika vitabu vya sheria.
3.         Sa’ayi: Hili ni zoezi la kwenda na kurudi mara saba baina ya vilima Swafaa na Mar-wa kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria.
4.         Kunyoa au kupunguza: Hili ni zoezi linalohusisha uondoshaji wa nywele zote kichwani au baadhi yake tu. Bora kwa mwanamume ni kunyoa na kwa mwanamke ni kupunguza kidogo tu.
 
 
B.       NAMNA YA KUHIJI:
 
F     Ikiwa wewe umechagua kuifanya ibada ya Hijjah kwa njia ya Ifraadi au Qiraani, basi hirimia Hijjah katika Miiqaati (Ihraamu sites) unayoingilia Makkah. Iwapo hauko katika Miiqaati, basi hirimia ulichokinuia mahala ulipo ndani ya mipaka ya Haram. Na ikiwa umechagua njia ya Tamatui, basi utahirimia Hijjah mahala ulipo siku ya Tarwiyah ambayo ni mwezi 8 Mfunguo tatu.
F     Baada ya kuhirimia, koga na ujitie manukato likikuwepesikia hilo. Kisha vaa vazi la Ihraamu, halafu sema: 
“LABBAYKA HAJJAN, LABBAYKAL-LAAHUMMA LABBAYKA, LABBAYKA LAA SHARIYKA LAKA LABBAYKA, INNAL-HAMDA WAN-NI’IMATA LAKA WAL-MULKU LAA SHARIYKA LAKA”.
F     Halafu ondoka uelekee Minaa na uswali hapo swala za Adhuhuri, Alasiri, Maghribi, Ishaa na Alfajiri ya mwezi tisaa. Utazikusuru swala za rakaa nne kwa kuziswali rakaa mbili mbili katika nyakati zake bila ya kuzijumuisha.
F     Litakapochomoza jua mwezi tisaa Mfunguo tatu, ondoka Minaa na uelekee katika viwanja vya Arafah kwa utulivu bila ya kuwaudhi mahujaji wenzio. Utaswali hapo swala za Adhuhuri na Laasiri kwa kuzijumuisha mjumuisho wa kutanguliza na kuzikusuru (yaani kuziswali rakaa mbili mbili badala ya nne nne). Ni wajibu uhakikishe kuwa umeingia na umo ndani ya mipaka ya Arafah, uwe makini sana khususan upande wa Kaskazini na Mashariki. Arafah yote ni mahala pa kusimama isipokuwa mahala panapoitwa “Batwni Arinah”. Ni kheri kwako ikiwa utafahamu kwamba kusimama Arafah ndio nguzo kuu ya Hijjah kutokana na kauli yake Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie: “Hijjah ni Arafah”. Kutokana na kauli hii ya Mtume wa Allah itakuwazikia kwamba mtu ambaye hakusimama katika viwanja vya Arafah mchana baada ya swala ya Adhuhuri au usiku mpaka kuchomoza kwa Alfajiri ya siku ya kuchinja (mwezi 10), hana Hijjah mtu huyo. Cha kufanya hapo Arafah ni kukithirisha mno kuleta adhkaari na dua, ilhali umeelekea Qiblah ukiwa umenyanyua mikono yako kama alivyofanya Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie. Endelea kubakia hapo Arafah mpaka kuchwa kwa jua.
F     Jua likishazama, shika njia kuelekea Muzdalifah kwa upole na utuvu mkubwa huku ukileta Talbiyah na tahadhari usiwaudhi mahujaji wenzako: “...NA MTAKAPORUDI KUTOKA ARAFAATI MTAJENI (mdhukuruni) ALLAH PENYE MASH’ARIL HARAAM...” [2:198] Utaswali hapa Muzdalifah swala za Maghribi na Ishaa kwa kuzijumuisha mjumuisho wa kuakhirisha, yaani uziswali swala mbili hizo zote; Maghribi na Ishaa katika wakati wa Ishaa. Utaziswali kwa adhana moja na Iqaamah mbili; Iqaamah moja kwa ajili ya Maghribi na nyingine kwa ajili ya Ishaa. Utabakia hapa mpaka kuswali Alfajiri ukikithirisha dhikri na dua.
F     Kisha ondoka kabla ya kuchomoza kwa jua la siku hii ya mwezi 10 Mfunguo 3; siku ya Eidil-Adh-haa uelekee Minaa huku ukileta Talbiyah. Ukiwa una udhuru, mathalan umeambatana na wanawake au madhaifu (wakongwe, walemavu n.k.) si vibaya ikiwa utaanza kuelekea Minaa tangu baada ya saa sita usiku. Chukua hapa Muzdalifah vijiwe saba (pebbles) kwa ajili ya kwenda kutupia  “Jamratul-Aqabah”, vijiwe vingine utachukua huko huko Minaa.
F     Ukishafika Minaa unatakiwa kufanya mambo yafuatayo:
1.      Kitupie/kipige mawe kinara cha Jamratul-Aqabah, hiki ni kile kilicho karibu na Makkah. Utakipiga mawe saba, yenye kufuatana moja baada ya jingine huku ukileta Takbiri na sio kuyatupa yote kwa mkupuo mmoja tu.
2.      Chinja mnyama (hadyu) ikiwa umelazimikiwa kutokana na kuifanya ibada ya Hijjah na Umrah kwa njia ya Tamatui au Qiraani. Ule sehemu ya nyama hiyo wewe mwenyewe na iliyobakia walishe mafakiri.
3.      Nyoa au punguza nywele, lakini kunyoa ni bora zaidi kwa mwanamume na mwanamke yeye atapunguza nywele kiasi kidogo tu.
Baada ya kutupia mawe Jamratul-Aqabah na kunyoa au kupunguza utakuwa umepata Tahalul ya kwanza, yaani utakuwa umepata uhalali wa kuyafanya yale yote uliyokuwa umezuiwa kwa sababu ya Ihraamu ila kumuingilia mkeo.
4.      Kisha teremka Makkah na utufu “Twawaaful-Ifaadhwah” mara saba, hii ni Twawaafu ya nguzo, kwani Hijjah yako haitimii ila kwa kuileta/kuitenda. Halafu ufanye Sa’ayi baina ya Swafaa na Mar-wa mara saba, hii ni iwapo ulichagua kufanya ibada mbili hizi; Hijjah na Umrah kwa njia ya Tamatui. Kadhalika kutampasa kufanya Sa’ayi yule aliyeichagua njia ya Qiraani au Ifraadi, iwapo hakufanya Sa’ayi baada ya Twawaful-Quduum. Baada ya Sa’ayi hii, ndipo utapata Tahalul ya pili ambayo itakuhalalishia mambo yote hata kumuingilia mkeo.
5.      Baada ya kutufu Al-Ka’abah Twaaful-Ifaadhwah siku ya kuchinja, rejea Minaa na ulale hapo usiku wa mwezi 11, 12 na 13 (masiku ya kuanika nyama – Ayyaamut-tashriyq). Kunajuzu pia kulala nyusiku mbili tu, yaani usiku wa mwezi 11 na 12. Hapa utavitupia mawe vinara vyote vitatu kila siku baada ya kupinduka jua, kila kinara utakitupia mawe saba; moja baada ya jingine huku ukileta Takbira kwa kila jiwe unalotupa. Utaanza kukitupia mawe kinara cha kwanza, siku ya mwezi 11, hiki ni kile kinachouandamia msikiti wa Hunayfi. Kisha utakitupia kinara cha kati na utamalizia na Jamratul-Aqabah. Utafanya hivi katika siku inayofuatia, yaani mwezi 12. Ikiwa una haraka, utaondoka kuelekea Makkah baada ya kuvitupia mawe vinara siku hiyo ya mwezi 12. Kuondoka huku ni sharti kuwe kabla ya kuzama kwa jua, ikiwa utachelewa mpaka jua likazama ukawa bado haujaondoka Minaa, basi kutakulazimu kulala hapo hapo Minaa na uvitupie mawe vinara baada ya kupinduka kwa jua siku ya mwezi 13. Hapo sasa ndio unaweza kuondoka Minaa kurudi Makkah: “NA MTAJENI ALLAH KATIKA ZILE SIKU ZINAZOHISABIWA, LAKINI AFANYAYE HARAKA KATIKA SIKU MBILI (akarejea) BASI SI DHAMBI JUU YAKE, NA MWENYE KUKAWIA PIA SI DHAMBI JUU YAKE, KWA MWENYE KUMCHA ALLAH...” [2:203] Baada ya kumaliza amali zote hizi za ibada ya Hijjah na Umrah na ukaazimia kufunga safari ya kurudi nyumbani, kunakuwajibikia kutufu “Twawaaful-Wadaai” ambayo hasameheki kuiacha ila mwanamke mwenye damu ya hedhi au nifasi tu. Mpaka hapa utakuwa umeikamilisha Hijjah yako.
 
Nguzo za Hijjah.
 
Ibada ya Hijjah imesimama juu ya nguzo zifuatazo:
1.         Kuhirimia.
2.         Kutufu “Twawaaful-Ifaadhwah”,
3.         Kusa’ayi baina ya Swafaa na Mar-wa.
4.         Kusimama Arafah.
5.         Kunyoa au kupunguza.
 
Waajibaati za Hijjah.
 
1.         Kuhirimia katika Miiqaati.
2.         Kulala Muzdalifah usiku wa Idi.
3.         Kulala Minaa katika masiku ya Tashriyq.
4.         Kutupia mawe vinara.
5.         Kutufu “Twawaaful-Wadaai”.
6.         Kujiepusha na Muharamaati za Ihraamu (mambo yaliyo haramishwa kwa sababu ya Ihraamu).
7.         Kunyoa au kupunguza.
Elewa na uzingatie kwamba Haji akiacha mojawapo ya nguzo za Hijjah, Hijjah yake hiyo haitasihi kisheria ila kwa kuitenda hiyo nguzo aliyoiacha. Na akiacha mojawapo ya Waajibaati zake, Hijjah yake itasihi lakini kutamlazimu kuchinja mnyama Makkah.
 
Yanayomuwajibikia mwenye kuhirimia.
 
Yanamuwajibikia mtu mwenye kuhirimia ibada ya Hijjah na Umrah mambo yafuatayo:
1.         Ajilazimishe kuyatenda yale yote aliyowajibishiwa na Mola wake katika fardhi za dini yake kama vile kuswali swala kwa nyakati zake tena katika jamaa.
2.         Ajiepushe na yale yote aliyokatazwa na Allah, asiseme maneno machafu, asifanye vitendo vichafu (ufasiki), asifanya mjadala muovu utakaopelekea uadui, na..... na......
3.         Ajiepushe na Muharaamati za Ihraamu (things unlawful while in Ihraam). Mambo yanayomuharamikia mwenye kuhirimia kwa sababu ya huko kuhirimia kwake Hijjah ni kama yafuatayo:
a)         Kunyoa/kukata nywele au kucha hata kidogo tu.
b)        Kujitia manukato mwilini au nguoni. Haidhuru athari ya manukato aliyojitia kabla ya kuhirimia.
c)         Kuwinda na kumuua mnyama au ndege wa bara au kumsaidia mtu kufanya hivyo.
d)        Kukata au kung’oa mimea ya Haram.
e)         Kuposa au kufunga ndoa yeye mwenyewe au kwa ajili ya mtu mwingine.
f)          Kumuingilia mkewe.
Haya yanawakhusu wote; mwanamume na mwanamke. Haya yafuatayo yanamkhusu mwanamume tu:
a)      Kufunika kichwa chake kwa kuvaa kitu mithili ya kofia au kilemba. Ama kutumia mwavuli si vibaya.
b)     Kuvaa nguo zilizoshonwa (sewn garments).
Ama mwanamke, yeye anakhusika na yafuatayo:
a)      Kuvaa gloves mikononi.
b)     Kufunika uso.
Kunajuzu kwa mwenye kuhirimia kuvaa kandambili/viatu, pete, miwani, saa na mkanda wa kuhifadhia pesa.

No comments: