Sunday, May 5, 2013

VURUGU ZAWAFIKISHA WAUMIN WA MORAVIAN POLISI

WAUMINI wa Kanisa la Moravian Kimara, jimbo la Misheni ya Mashariki, wilayani Kinondoni, jana walishindwa kufanya ibada, kutokana na vurugu kubwa iliyozuka kanisani hapo na kusababisha baadhi ya waumini na viongozi kufikishwa katika kituo cha polisi Mbezi.
Wakati baadhi ya waumini na viongozi wa kanisa hilo wakifikishwa kituoni, mchungaji msaidizi wa kanisa hilo anayelalamikiwa kung’angania madaraka, Fani Ndemange, aliamuru waumini wanaomsikiliza kuwafukuza waandishi wa habari waliofika kanisani hapo kutaka kujua chanzo cha ibada hiyo kutofanyika.
Wakati Mchungaji Ndemange akionyesha kutokutaka taarifa hizo zijulikane kwa umma, waumini wengine waliokuwa wakimshinikiza aondoke kanisani hapo walisema chanzo cha mgogoro huo ni kuhoji uhalali wa kuongozwa na mchungaji huyo ilhali ni miongoni mwa wachungaji 14 wa kanisa hilo waliofukuzwa na kutakiwa kutojihusisha na suala lolote la kanisa hilo.
“Hii ni wiki ya nne ibada yetu inasimamiwa na polisi na sababu kubwa ni hawa viongozi waliofukuzwa kugeuza kanisa kama taasisi yao; tazama leo huyu mchungaji kaja kusaidiwa na mumewe kulazimisha kutuongoza wakati sisi hatumtaki na uongozi wa juu ulishamuondoa,” alisema Mwaikambo aliyejifahamisha kama muumini wa kanisa hilo.
Muumini mwingine alisema baada ya Mchungaji Msaidizi Ndemange kuona mabango yanayotaka afafanue matumizi ya zaidi ya sh milioni 23 alipiga simu polisi na kusema ametishiwa kumwagiwa tindikali na kwamba baadhi ya waumini wana silaha za moto.
“Walikuja askari wakiwa na gari DFP 891 Landcruise Toyota wakazuia ibada isiendelee huku wakiwachukua baadhi ya waumini na viongozi kwenda nao kituo cha polisi,” alisema muumini mwingine.
Habari kutoka kanisani hapo zilieleza kuwa vurugu hizo zilisababishwa na wafuasi wa baadhi ya wachungaji 14 waliofukuzwa na uongozi wa Kanisa la Moravian Tanzania (KMT), Jimbo la Kusini mwanzoni mwa mwaka jana.
Wachungaji hao wakiongozwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Jimbo la Misheni, Mchungaji Clement Fumbo, walifukuzwa na uongozi wa kanisa hilo kutokana na makosa yanayodaiwa kuwa ni utovu wa nidhamu pamoja na kujitangazia halmashauri kuu kinyume na katiba ya kanisa hilo.

No comments: