Sunday, May 5, 2013

UN yataka maalbino Tanzania walindwe

Nchini Tanzania Mei nne ni siku ya kitaifa ya Albino ambapo jopo la wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wametaka mamlaka zote husika kuzuia mauaji ya Albino na uchunguzi wa kina ufanyike dhidi ya watekelezaji wa vitendo hivyo.  Mmoja wa wataalamu hao Juan E. Méndez amesema utekelezaji wa vitendo vyovyote vya kikatili hauwezi kuhalalishwa na kwamba kwa mujibu wa sheria za kimataifa ni jukumu la serikali kuwapatia albino ulinzi dhidi ya wale wanaotaka kuwaua. Ametoa kauli hiyo kutokana na kuwepo kwa taarifa za mauaji ya albino na viungo vyao kutumiwa kwa imani potofu za kishirikina nchini Tanzania na katika baadhi ya nchi barani Afrika. Mtaalamu mwingine wa Umoja wa Mataifa, Kishore Singh ambaye anahusika na elimu amesema kuwepo kwa siku ya kitaifa nchini Tanzania ni fursa kubwa ya kumulika tatizo hilo na kuibua mjadala kuhusu masaibu yanayowakumba albino nchini humo.

No comments: