Naibu Waziri wa Ujenzi, Gerson Lwenge, amegeuka mbogo baada ya mmoja wa
wamiliki wa magari ya mizigo kumwambia amewadanganya wabunge kuwa
hafahamu ucheleweshaji wa vibali vya magari ya kunyanyulia vitu vizito.
Aidha, Mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage, (CCM), aeleza jinsi
alivyozomewa na wakazi wa Mkoa wa Morogoro, baada ya watu wawili
waliobanwa katika ajali kushindwa kuokolewa kwa sababu ya kukosekana kwa
vifaa.
Hali hiyo ilitokea juzi wakati Chama cha Wamiliki wa Magari ya Mizigo
(Tatoa), walipokutana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu pamoja
na mawaziri.
Mawaziri waliohudhuria mbali ya Lwenge, ni Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk.
Charles Tizeba na Naibu Waziri wa Fedha, Janeth Mbene. Baada ya Tatoa
kuelezea kero zao kuhusu sekta ya usafirishaji, mawaziri walipewa nafasi
ya kujibu kero hizo na Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu, Peter
Serukamba.
Lwenge alisema suala la rushwa katika mizani ambalo linalalamikiwa na
chama hicho linahusu pande mbili yaani mtoaji na mpokeaji. Kuhusu vibali
vya magari ya kubebea vitu vizito kuchukua muda mrefu, aliwataka kwenda
ofisini kwake kuzungumza naye iwapo kuna tatizo hilo. Wakati akiendelea
kuelezea ndipo mmliki huyo aliposimama na kusema kuwa waziri
amedanganya hadhara hiyo kwa kuwa wameshapeleka malalamiko hayo kwa
maandishi mara kadhaa bila ufumbuzi.
Maneno hayo yalionekana kumkera sana Lwenge na kuja juu akimtaka mmiliki
huyo kumsikiliza na yeye. Hata hivyo, Dk. Tizeba aliingilia kwa kusema
wao kama serikali wameyasikia na kuwa watakaa na kuyatafutia ufumbuzi wa
kero hizo na kisha kuwajibu.
Kuhusu kero ya matuta, Lwenge alielezea kuhusiana na kero ya matuta
yaliyowekwa katika barabara, alisema tayari wameshaanza kuondoa matuta
yasiyo na viwango ambayo yamekuwa ni kero kwa wasafirishaji.
Hata hivyo, alikumbana na swali kutoka kwa Serukamba likimtaka atoe
mfano wa barabara ambazo matuta yameondolewa na ndipo alipotaja barabara ya Dar es Salaam kwenda Dodoma.
“Mimi Mheshimiwa waziri nimepita hapo juzi, matuta yapo vile vile,”
alisema Serukamba, hali iliyomfanya waziri kubadilisha kauli yake kwa
kukiri kuwa hayajaondolewa.
Kuhusu msongamano katika mpaka wa Tunduma, Dk. Tizeba, alisema ujumbe
wa Tatoa na serikali utaondoka kwenda Zambia Mei 7 kujadiliana. Mwijage
aliitaka serikali kuchukua hatua ya kununua vifaa vya kuokolea wakati
inapotokea ajali. “Nilipita pale nikakuta kuna ajali imetokea watu
wamebanwa na vyuma wameshindwa kuokolewa, walipogundua kuwa mimi ni
mbunge nilizomewa ilikuwa ni aibu,” alisema.
Mbunge mwingine aliitaka serikali kuangalia risiti zinazotolewa
bandarini kwa kuwa watu huandikiwa katika vikaratasi wanapotozwa fedha.
Mbunge wa Gairo, Ahmed Shabiby (CCM), alishangazwa na hatua ya serikali
kuweka mizani mingi njiani wakati gari linapoondoka bandarini linapimwa
na kufungwa vizuri.
Pia alikerwa na tabia ya kampuni za udalali ya Yono na Majembe, ambazo
alisema zimekuwa zikiwabughudhi wamiliki wa magari hayo kwa kuyakamata
ovyo.
No comments:
Post a Comment