Sunday, May 5, 2013

Shambulio jipya la utawala haramu wa Kizayuni huko Syria

Kwa mara nyingine duru mbalimbali za habari, zikiwemo za utawala haramu wa Kizayuni wa Israel, zimetangaza habari ya utawala huo kufanya mashambulizi nchini Syria. Shirika la Habari la Syria (SANA) limetangaza leo kuwa, asubuhi ya leo kulisikika sauti ya miripuko kadhaa karibu na eneo la Alhama lililoko katika viunga vya mji mkuu wa nchi hiyo Damascus. Taarifa za awali zilizotangazwa zinaeleza kuwa, kituo cha utafiti kilichoko katika eneo la Jamraya na ambacho pia kilishambuliwa na utawala huo katika miezi ya hivi karibuni, ni miongoni mwa maeneo yaliyoshambuliwa leo na ndege za utawala wa haramu wa Kizayuni wa Israel. Kituo cha habari cha Syria pia kimetangaza habari ya kutokea miripuko katika maeneo tofauti ya mji wa Damascus. Inasemekana kwamba, miripuko hiyo imetokea katika kambi ya jeshi la kikosi nambari nne iliyoko katika eneo la Mount Qasioun na katika kituo cha utafiti cha Jamraya. Aidha duru za habari zimetangaza habari ya kusikika sauti za milipuko katika kikosi nambari 105 cha gadi ya rais wa Syria. Wakati huo huo, vyombo vya habari vya Syria vimetangaza kuwa, kombora la kwanza lililotupwa na ndege za utawala katili wa Kizayuni katika eneo la Jamraya, lilikuwa na mada za urani khafifu. Miripuko, mashambulio na ukiukaji wa hivi sasa wa anga ya Syria, unajiri katika hali ambayo, mwezi Januari mwaka huu, ndege za kijeshi za Israel zilikishambulia pia kituo cha utafiti cha Jamraya katika viunga vya mji mkuu wa Syria, Damascus. Baadhi ya duru za kisiasa zimetangaza kuwa, mashambulizi mapya ya Israel nchini Syria, yanabainisha wazi kuwa, utawala huo unaingilia moja kwa moja mgogoro unaoendelea nchini humo na kwamba, makundi ya kigaidi yanayofanya mauaji ya raia huko Syria hayawezi kukanusha mahusiano yake ya moja kwa moja na njama hizo za Israel. Chanzo kimoja cha habari pia kimesisitiza kuwa, mashambulizi ya anga ya ndege za Kizayuni huko Damascus na ambayo yamefanyika baada ya kushindwa makundi ya kigaidi yanayofadhiliwa na madola ya kigeni, kukabiliana na jeshi la Syria, ni njama zenye lengo la kuandaa mazingira ya kuyapenyeza makundi ya kigaidi mjini humo. Ushahidi wa hayo ni kuwa, muda mchache tu tangu ya kufanyika mashambulizi hayo ya Wazayuni, jeshi la Syria lilifanikiwa kufelisha njama za magaidi waliokuwa na nia ya kujipenya zaidi mjini Damascus kwa ajili ya kufanya uharibifu na jinai nyenginezo. Kwa upande wake Tony Cartalucci, mchambuzi wa masuala ya kisiasa na mwandishi wa habari raia wa Thailand ameyataja mashambulizi hayo ya utawala katili wa Kizayuni mjini Damascus kuwa yanaashiria ni namna gani Wamagharibi walivyoshindwa na taifa hilo la Kiarabu. Amesisitiza kuwa, hatua hiyo inaonyesha kwamba makundi ya kigaidi huko Syria ambayo yamelelewa na Marekani, Israel na Saudi Arabia, yameshindwa kabisa kuiangusha serikali halali ya Rais Bashar al-Assad, hivyo yanahitaji msaada wa uingiliaji kijeshi wa Washington na washirika wake wa eneo hili. Ni wazi kwamba, mashambulizi hayo ya ndege za Israel yamefanyika kwa msaada kamili wa Marekani ikiwa ni katika njama na mipango iliyosukwa na Marekani yenyewe. Hii ni katika hali ambayo, serikali halali ya Syria imetoa onyo kali kwa utawala huo bandia na kusisitiza kuwa, jeshi la nchi hiyo litajibu kila chokochoko za utawala wa Kizayuni katika wakati mwafaka. Wakati huo huo, Russia nayo pia imeonya kuhusu uvamizi wowote ule wa kijeshi wa nchi za Magharibi dhidi ya Syria.

No comments: