Sunday, May 5, 2013

Maduro: Barack Obama ni rais wa mashetani

Rais Nicolas Maduro wa Venezuela amemshambulia vikali Rais Barack Obama wa Marekani na kuwita kuwa ni rais wa mashetani. Maduro ametoa matamshi hayo makali dhidi ya Obama baada ya rais huyo wa Marekani kuhojiwa na kanali moja ya televisheni ya lugha ya Kihispania. Akihojiwa na kanali ya televisheni ya Univision, Obama alikataa kusema iwapo anamtambua Maduro kuwa ni rais halali wa Venezuela au la. Vile vile Obama ameuita mrengo unaotawala nchini Venezuela kuwa ni wa kifashisti. Akijibu matamshi hayo ya Obama, Rais wa Venezuela amesema kuwa, kazi yetu sisi ni kulinda taasisi zetu, amani na demokrasia ya wananchi wa Venezuela na tunaweza kukaa na kila mtu, hata kiongozi mkuu wa mashetani. Vile vile Rais Maduro amemlaumu vikali rais huyo wa Marekani kwa kuwasaidia kifedha wapinzani nchini Venezuela. Maduro amesema pia kwamba, ni Obama mwenyewe ambaye ni kitimbakwiri cha madola ya kibeberu ndiye aliyetoa fedha nyingi kuusaidia kifedha mrengo wake ambao lengo lake kubwa ni kuiangamiza Venezuela. Tarehe 14 mwezi uliopita wa Aprili, Maduro alichaguliwa na wananchi wa Venezuela kuiongoza nchini hiyo, jambo ambalo limewahamakisha sana viongozi wa Marekani ambao wanashindwa kuficha hamaki zao.

No comments: