Monday, September 8, 2014

Di Maria aibua zengwe Madrid

MADRID, HISPANIA
WINGA, Angel Di Maria ameibua jipya kuhusu klabu yake ya zamani ya Real Madrid.
Staa huyo mpya wa Manchester United raia wa Argentina amefichua kwamba Real Madrid ilimtumia barua siku ya fainali ya Kombe la Dunia nchini Brazil ikimtaka asicheze mechi hiyo.
Alibainisha kwamba amekuwa hana uhusiano mzuri na rais wa klabu hiyo, Florentino Perez, mtu ambaye hasa ndiye anayepaswa kubeba lawama kutokana na kuondoka kwake  katika Uwanja wa Bernabeu katika dirisha la usajili lililomalizika karibuni.
“Nilipata barua kutoka Real Madrid, ilinifikia saa 5 asubuhi ilikuwa ni siku ya fainali ya Kombe la Dunia na ilielezea kuwa nisicheze mechi hiyo,” alisema winga huyo.
“Mechi ilikuwa saa 10 jioni na nilikuwa najiandaa kujiweka vizuri kwa sababu nilikuwa nimeumia. Mawazo yangu yalikuwa ni kucheza mechi ya fainali, ingawa nilifahamu hilo lilikuwa na asilimia 90 tu.
“Mara nikapata barua hiyo na niliichapa.  Sikujali kitu kwa chochote ambacho kingetokea. Nilipata mawazo mengi  asubuhi ile na kusema nini hiki kimetokea kwenye maisha yangu. Sikumwambia yeyote pale klabuni kwa kuwa sikutaka maoni ya mtu mwingine bali nilitaka kutafakati mwenywe.”
Di Maria aliongeza: “Nilikuwa na uhusiano safi tu na wachezaji wenzangu. Sikuwa vizuri na Florentino Perez. Niliposaini mkataba wangu klabuni hakuwapo.”

Okwi ajibu makelele ya Yanga

STRAIKA wa Simba, Emmanuel Okwi,  anajiamini kupita kiasi na akawaambia mashabiki wa Yanga, waendelee kumzomea hivyo hivyo, kwani kelele zao zinaingilia kulia na kutokea kushoto na mwisho wa siku watampenda tu.

Okwi raia wa Uganda, ana utata na Yanga ambayo ana mkataba nayo lakini ameukana mkataba huo na kusaini Simba kutokana na sababu mbalimbali ambapo juzi Jumamosi aliichezea kwa mara kwanza klabu hiyo ya Msimbazi kwenye mechi ya kirafiki waliyoifunga Gor Mahia mabao 3-0.
Katika mchezo huo, Okwi alipata tabu kutoka kwa mashabiki wa Yanga ambao kila alipogusa mpira walikuwa wanamzomea jambo ambalo limeelezwa na wadau wengi wa soka kuwa litamfanya ashindwe kucheza mpira.
Lakini alipozungumza na Mwanaspoti, Okwi alisema: “Hiyo zomea zomea yao, watazomea sana lakini kamwe hawataweza kunifanya nishindwe kucheza mpira.
“Mimi ni mchezaji mkubwa, najielewa, hicho wanachikifanya ni kujisumbua tu, nitacheza na kupiga mabao kama kawaida na wakibisha wataona.”
 Beki wa Yanga, Mbuyu Twite, ambaye awali alikuwa kwenye rada ya Simba aliwahi kukumbana na zomea zomea ya Simba waliokuwa wakimkejeli kwa kumuita mwizi kwa madai kwamba alichukua fedha zao za usajili akaingia mitini.
Tofauti na Twite ambaye alikuwa akiwajibu kwa ishara mbalimbali akiwa uwanjani, Okwi alifanya jambo dogo sana ambapo kila alipokuwa akiitwa jina hilo alikuwa akiwanyooshea dole mashabiki wa Simba ambao walijibu kwa kumshangilia kwa nguvu jambo lililoleta raha.
Kocha Mkuu wa Simba Patrick Phiri amefurahishwa na uwezo ulioonyeshwa na Okwi lakini akampa jukumu moja kubwa ambalo anatakiwa kulikamilisha mapema ili aweze kutisha.
“Namjua Emmanuel (Okwi) ni kijana mzuri, lakini amenifurahisha sana na uwezo aliouonyesha amecheza vizuri kwa kiasi chake lakini bado ananafasi ya kufanya vizuri zaidi,” alisema Phiri.
“Bado hayupo sawa sana, lakini hilo lipo mikononi mwake. Kuhakikisha anajituma zaidi mazoezini, anaweza kuwa sawa zaidi endapo atajituma kufanya mazoezi ya nguvu.
“Kama akifanikiwa hilo atarudi katika uwezo na kuweza kuisaidia Simba.”

DALADALA ZAGOMA KUTOA HUDUMA MANISPAA YA IRINGA

KITUO CHA MABASI MIYOMBONI KUKIWA HAKUNA DALADALA HATA MOJA BAADA YA KUGOMA

STENDI YA MASHINE TATU ABIRIA WAKISUBIRI DALADALA BAADA YA KUGOMA KUTOA HUDUMA
BAADHI YA ABIRIA WAKILAZIMIKA KUTUMIA USAFIRI WA TOYO BAADA YA DALADALA KUGOMA



MADEREVA wa daladala manispaa ya Iringa leo wameanza mgomo “usio na kikomo” wakizishinikiza mamlaka zinazohusika kuwazuia madereva wa pikipiki za miguu mitatu “Bajaj” kufanya biashara ya daladala. 
Hatua hiyo imeleta adha kubwa kwa watumiaji wa usafiri wa daladala japokuwa imekuwa neema kubwa kwa waendesha bodaboda, Bajaj na malori madogo aina ya Suzuki Carry. 
Wakizungumzia mgomo huo, baadhi ya wakazi wa mjini hapa wamesema kwamba umewaathiri kwa kiasi kikubwa huku wakiutupia lawama uongozi wa mamlaka ya usafiri wan chi kavu na majini (SUMATRA) mkoa wa Iringa.
Aidha mmoja wa madereva wa daladala hao ambaye hakutaja jina lake amesema kuwa tatizo hilo la mgomo ni kutokana na utaratibu mbovu wa waendesha bajaji.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama cha wasafirishaji kwa kutumia pikipiki mkoa wa Iringa Bw. Joseph Mwambabe, amewatupia lawama viongozi wa Sumatra kwa kuuchochea mgomo huo
Hata hivyo Mwambabe  amesema tatizo hilo wamelifikisha katika ofisi za mkuu wa mkoa na mpaka sasa wanasubiri unatatibu utakao waongoza katika kazi zao.
 Mgomo huo umechukua zaidi ya masaa 10 kuanzia saa kumi na mbili hadi habari hii inatumwa ulikuwa bado ukiendelea Mjengwablog lilimtafuta Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani Leopord Fungu ofisini kwake alikuwa katika kikao pamoja viongozi wa kamati ya usalama barabarani kwa kushirikiana na uongozi wa Sumatra mkoa wa Iringa.

`Kujiuzulu mwanasheria wa Zanzibar hakutaathiri Bunge`

Bunge Maalum la Katiba limesema kujiuzulu kwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar katika Kamati ya Uandishi wa Katiba mpya hakutaathiri upatikanaji wa katiba mpya.

Katibu wa Bunge hilo, Yahya Khamis Hamadi, alisema kitendo cha kujiuzulu kwa mwanasheria mkuu, Othman Masoud Othman, ni jambo la kawaida na kwamba uwakilishi wa Zanzibar ndani ya chombo hicho utakuwepo.

Alisema hajapata taarifa rasmi ya kujiuzulu kwa Othman katika kamati hiyo ambayo ipo chini ya Uenyekiti wa Mbunge wa Bariadi Mashariki, Adrew Chenge, lakini kama amefanya hivyo atakuwa ametimiza wajibu wake kisheria.

Hamad, alisema kwamba mwanasheria huyo hakuingia katika Kamati ya uandishi wa Katiba mpya kutokana na wadhifa wake, bali ni uteuzi wake ulifanywa na uongozi wa Bunge hilo kama wajumbe wengine.

Katibu huyo aliongeza kuwa uwakilishi wa Zanzibar katika kamati hiyo utakuwepo kwa sababu kuna wajumbe wengine kutoka upande huo wa Muungano wanaendelea na kazi hiyo kikamilifu.
 

BENKI KUU YATOA SARAFU YA SH.500

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetangaza kutoa toleo jipya la sarafu ya Sh. 500, inayotarajiwa kuingizwa kwenye mzunguko na kutumika rasmi kama fedha halali nchini, kuanzia mwezi ujao.

Hatua hiyo imechukuliwa na BoT kwa kuzingatia sababu mbalimbali, ikiwamo noti ya Sh. 500 iliyopo sasa kwenye mzunguko kupita kwenye mikono ya watu wengi katika kipindi cha muda mfupi na hivyo, kuchakaa haraka.

Mkurugenzi wa Huduma za Kibenki wa BoT, Emmanuel Boaz, aliwaambia waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana kuwa sarafu hiyo itakuwa ikitumika sambamba na noti zilizopo za Sh. 500 mpaka hapo noti hizo zitakapokwisha katika mzunguko.

“Hatua hii imezingatia kwamba, noti ya Sh. 500 ndiyo inayotumika zaidi kwenye manunuzi ya kawaida ya kila siku ya wananchi wengi kuliko noti nyingine yoyote. Hivyo, noti hiyo hupita kwenye mikono ya watu wengi katika kipindi cha muda mfupi sana na kuchakaa haraka,” alisema Boaz.

Alitaja sababu nyingine iliyozingatiwa katika kutoa sarafu hiyo kuwa ni noti hizo (za Sh. 500) kukaa katika mzunguko kwa muda mrefu bila kurejeshwa kwenye mabenki kwa wakati muafaka ili zibadilishwe zinapokuwa zimefikia ukomo wake.

Sababu nyingine ni sarafu kuwa na uwezo wa kukaa kwenye mzunguko kwa miaka mingi (zaidi ya miaka 20) zaidi kuliko noti.

Alisema sarafu hiyo ina umbo la duara lenye michirizi pembezoni, kipenyo cha milimita 27.5 na uzito wa gramu 9.5, ina rangi ya fedha na imetengezwa kwa madini aina ya chuma na “Nickel”.

Pia upande wake wa mbele ina sura ya Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Sheikh Abeid Aman Karume, na kwa nyuma ina taswira ya mnyama nyati akiwa mbugani.

Vilevile, ina alama maalumu ya usalama iitwayo “latent image”, iliyopo upande wa nyuma, ambayo ni kivuli kilichojificha, ambacho huonesha thamani ya sarafu “500” au neno BoT inapogeuzwageuzwa.

Sunday, April 27, 2014

MKAKATI WA SERIKALI YA UMOJA WA KITAIFA PALEST. WAANZA

Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina hivi karibuni ataanzisha mazungumzo na pande husika kwa minajili ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa huko Palestina. Taarifa zinasema kuwa, Mahmoud Abbas anakusudia kukutana na makundi na shakhsia mbalimbali huru ili kujadiliana nao kuhusu mchakato wa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa. Taarifa zinasema kuwa, Abbas atajadiliana na makundi na shakhsia hao kuhusiana na mawaziri watakaounda serikali ya umoja wa kitaifa, na kisha kuandaa mazingira ya kuitishwa uchaguzi wa rais na bunge. Duru za kisiasa zinaeleza kuwa, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ana mpango wa kuunda serikali itakayowashirikisha shakhsia huru na wasiofungamana na mirengo ya kisiasa, akihofia radiamali itakayotolewa na utawala wa Kizayuni wa Israel na Marekani. Inafaa kuashiria hapa kuwa, hivi karibuni harakati za Fat–h na Hamas zilitiliana saini makubaliano ya  kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa katika kipindi cha wiki tano zijazo, ambayo itasaidia kuondoa mivutano na mifarakano kati ya pande hizo mbili.

WAISLAMU 1300 WAUKIMBIA MJI WA BANGUI, CAR

Televisheni ya al Alam imetangaza leo kuwa, karibu Waislamu 1300 waliokuwa wamejificha katika eneo moja la pambizoni mwa mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Bangui, wamelazimika kulikimbia eneo hili kwa kuhofia kushambuliwa na wanamgambo wa Kikristo wa Anti-Balaka.
Taarifa zinasema kuwa Waislamu hao leo wameonekana wakiingia kwenye malori madogo 18 wakielekea maeneo ya kaskazini mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati chini ya usimamizi wa askari wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika, AU.
Televisheni ya al Alam imelinukuu shirika la habari la AFP likisema kuwa, mara baada ya malori yaliyowabeba Waislamu kuondoka sehemu hiyo, mamia ya wanamgambo wa Kikristo wa Anti-Balaka waliokuwa wanasubiri kwa hamu mita chache tu, wamelivamia eneo hilo ili kufanya wizi na uporaji dhidi ya mali za Waislamu hao.
Waislamu hao waliokuwa wamekimbia maeneo yao na kujificha katika eneo hilo, hawakusalimika na ukatili wa wanamgambo hao wa Kikristo ambao waliwazingira Waislamu hao hadi askari wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika walipofika na kuamua kuwahamisha katika eneo hilo.