Sunday, July 14, 2013

BAKWATA ARUSHA YALALAMIKIA UTENDAJI WA POLISI



Baraza Kuu la Waislamu nchini Tanzania BAKWATA limelalamikia jinsi wahusika wa mashambulizi yanayotokea mara kwa mara dhidi ya masheikh mkoani humo wasivyofuatiliwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Malalamiko hayo yametolewa na Kaimu Katibu wa Bakwata Mkoa wa Arusha, Sheikh Abdallah Masoud kufuatia shambulio la juzi la mtu asiyejulikana dhidi ya Shekhe Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Sheikh Said Juma Makamba aliyejeruhiwa vibaya kwa kumwagiwa maji yanayosadikiwa kuwa ni tindikali. 

Sheikh Makamba ameshambuliwa na mtu asiyejulikana akiwa nyumbani kwake jijini Arusha.

Akilaani tukio hilo, Sheik Abdallah Masoud amesema, ameshitushwa sana na tukio hilo na kusisitiza kuwa linafanana na shambulizi alilofanyiwa Katibu wa Bakwata Mkoa wa Arusha, Abdulaziz Jonjo ambaye mwaka jana aliripuliwa kwa bomu akiwa amelala nyumbani kwake.

Kaimu Katibu wa Bakwata Mkoa wa Arusha amesema, matukio hayo yamekuwa yakijirudia huku wahusika wakishindwa kutiwa mbaroni na kusisitiza kwamba, pamoja na kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi, lakini wamekuwa hawapati taarifa za kukamatwa watuhumiwa licha ya kwamba amesema wanajulikana.

Sheikh Mkuu wa Wilaya ya Arumeru anaendelea kupata matibabu katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru baada ya kujeruhiwa vibaya maeneo ya usoni, kifuani, mkononi na mgongoni.

Naye  Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas amesema, polisi wameanza uchunguzi wa tukio hilo ingawa hadi sasa hakuna  mtu anayeshikiliwa kuhusishwa na shambulio hilo.

No comments: